November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia aungwe mkono kwa uongozi wa haki

*Ni kauli ya walioachiwa baada ya kusota gerezani kwa kesi tuhuma za ufisadi wakipigwa kalende, watoa sadaka ya shukurani Krismasi, wamuombea

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

BAADHI ya Watut waliokuwa wakikabiliwa na kesi za uhujumu uchumi na ufisadi wamesema Rais Samia Suluhu Hassan, ameonesha kwa vitendo kuwa ni kiongozi anayesimamia utawala wa sheria, hatua ambayo imewawezesha kuungana na familia za kusherehekea Sikukuu ya Krismasi, mwaka huu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kutoa sadaka ya shukurani kanisani jana, Pugu, nje Kidogo wa jijini Dar es Salaam, walisema bila Rais Samia ni wazi hata sikukuu za mwaka huu zingewakuta gerezani.

“Leo mimi na wenzagu watatu tumekuja kutoa sadaka ya shukurani kumshukuru Mungu kwa aliyotutendelea kupitia uongozi wa Rais Samia. Tumekaa gerezani miaka minne hadi mitano.

Lakini leo tupo uhuru. Ndipo maana ndugu, jamaa na marafiki wametusindikiza kutoa sadaka ya shukurani,” alisema mmoja wa washtakiwa aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya kuhujumu uchumi.

Mwingine ambayo alikuwa amejumuishwa kwenye kesi hiyo akizungumza kwa sharti la jina lake kutochapishwa gazetini alisema;

“Kwa miaka mitano tumekaa Gerezani tukikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na ufisadi. Kesi zilikuwa zikiahirishwa mara kwa mara, lakini alipoingia madarakani Rais Samia alitaka kesi ambazo upande wa Jamhuri wanaona hawana ushahidi wa kutosha kuandelea nazo zifutwe.

Tuliposikia agizo la Rais tukiwa gerezani, tulijua wazi ukweli utajulikana. Wote tulichiwa baada ya DPP kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi,” alisema.

Alisema kesi zao zitajwa bila kusikilizwa kwa kile kilichokuwa kikidaiwa na upande wa mashtaka kutokamilisha ushahidi.

Alisema kwa kipindi cha miaka mitano ambayo wamekaa Gerezani, familia zao ziliyumba na hata watoto kushindwa kuendelea na masomo, hivyo anavyotokea kiongozi anayesimamia haki kwa vitendo ni lazima Watanzania wamuombee.

Aliwataka Watanzania wanapokumbana na majaribu kama yaliyowakuta, wasiache kumtanguliza Mungu pamoja na kumuombea Rais Samia aweze kuendelea kuongoza kwa haki.

“Mke wa mmoja wa washtakiwa hao ambao walisota gerezani, alisema kila siku walikuwa wanaomba Mungu aweze kutenda haki ili ukweli ujulikane na kupitia kwa Rais Samia hilo limewezekana,” alisema.

Alisema hata juzi Jumapili aliposikia Salam za Rais Rais Samia kwa Watanzania kwa ajili ya mwaka mpya alizipokea mikono miwili, kwani ni salamu za faraja.

Juzi Rais Samia kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii kwa Mwaka 2023 aliwataka Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa juhudi, weledi

“Nawatakia Watanzania wote kheri ya Krismasi na Mwaka Mpya. Tumpe Mwenyezi Mungu shukrani kwa kutufikisha salama wakati huu wa mwaka,” alisema Rais Samia kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Septemba, mwaka jana Rais Samia amemuagiza Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai, kuhakikisha unafanyika upelelezi na kuwa na ushahidi wa kutosha kabla ya kumweka mtuhumiwa mahabusu.

Alitoa agizo hilo mkoani Kilimanjaro alipokuwa anafungua kikao kazi cha maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao makuu na makamanda wa mikoa na vikosi.

Mara baada ya kauli hiyo ya Rais, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dkt. Edward Hoseah, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema mtu hastahili kupelekwa mahakamani kama upelelezi haujakamilika.

Dkt Hoseah alisema madhara ya kumpeleka mtu mahakamani kabla ya upelelezi kukamilika ni pamoja na kumuumiza kwa kumharibia heshima yake na kuifanya familia yake kuishi kwa wasiwasi wakati wote.

“Alichosema Mheshimiwa Rais ni sahihi, hata wakati wa kampeni zangu mwaka juzi nilikuwa nikilisema hili kwamba usimpeleke mtu mahakamani kabla hujakamilisha upelelezi, huu ndiyo msimamo wangu na ndiyo msimamo wa sheria,” alisema Dk Hoseah.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Tike Mwambipile alisema polisi hawapaswi kumkamata mtu kabla hawajakamilisha upelelezi, bali watafute kwanza ushahidi wa kujitosheleza ili mtu anapokamatwa apelekwe moja kwa moja mahakamani.

“Mtu anaathirika zaidi kisaikolojia hasa kwa yule ambaye hajatenda hilo kosa, hata kama anatoka nje kwa dhamana, lakini bado ni mtuhumiwa na jamii inajua kuwa ni mtuhumiwa,” alisema Mwambipile.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema kinachofanyika nchini ni kinyume kwa kuwa inatakiwa upelelezi ukamilike kwanza ndipo mtu akamatwe.

Henga alisema kama hakuna ushahidi mtu hapaswi kukamatwa na ndicho kitu alichosisitiza Rais Samia.

“Kitu kinachotakiwa kufanyika ni kurekebisha Sheria ya Makosa ya Jinai kwa sababu ina mapengo ikiwemo suala la upelelezi kwanza haisemi, pia ina mapengo kwenye makosa yasiyo na dhamana na yenye dhamana,” alisema Henga.

Alisema madhara ya upelelezi kuchelewa ni makubwa kwa kuwa haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa kwa kuwa kama mtu alitakiwa asikilizwe ndani ya siku 10 akasikilizwa ndani ya siku 100, anapata mateso kutokana na uzembe wa kutosikilizwa.

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto kupitia katika mtandao wa kijamii wa twitter alimshukuru Rais Samia na kusema kuwa hivi ndivyo inavyopaswa kuwa mtu asikamatwe bila ushahidi kukamilika.

Zitto alisema kauli hiyo ilete mabadiliko ya mfumo wa haki jinai ikiwamo kwa kila kosa kuwa na dhamana isipokuwa baadhi tu ukiwemo uhaini.