November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Salawe waishukuru Serikali kuwapatia maji kutoka ziwa Victoria

Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga

WAKAZI wa Kata ya Salawe katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wameishukuru Serikali kwa kuwapatia huduma ya maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria na kumaliza kabisa changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama katika maeneo yao.

Wakazi hao walisema kupatikana kwa maji ya uhakika kumepunguza kama siyo kumaliza kabisa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike walivyokuwa wakitendewa pindi wanapokwenda kutafuta maji kwenye visima na mito ambapo pia walitumia muda mrefu.

Wananchi hao wametoa shukrani zao juzi wakati wakizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti hili anayefuatilia utekelezaji wa mradi wa Sauti za Kaya na vyombo vya habari katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ukifadhiliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT).

“Kwa kweli sisi watu wa hapa Songambele Salawe, tunaishukuru na kuipongeza Serikali kwa kutupatia huduma ya maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria, ile kero tuliyokuwa nayo kwa kipindi kirefu sasa haipo tena, hata mama zetu kwa sasa ndoa zao ziko salama,” alieleza Ramadhani Masonoku mwenyekiti wa kitongoji cha Songambele.K

wa upande wao Naomi George, Witness Simbila na Verediana Selestine walisema awali kabla ya maji kutoka Ziwa Victoria walikuwa na shida kubwa ya maji ambapo walilazimika kuamka saa 10 alfajiri kwenda mtoni kuchota maji ambako pia yalikuwa ya kusubiria.

“Tulikuwa na visima vya kusukuma kule bondeni, lakini maji yake hayakuwa mazuri sana, hivyo wengi ilibidi tuamke usiku kwenda mtoni kwa ajili ya kupata maji ambayo hayakuwa na chumvi, sasa kutokana na idadi ya watu kuwa wengi ilibidi kuamka usiku, kwa sisi wenye kuolewa ilikuwa shida,”

“Ilipotokea umechelewa kurudi, lazima mwanamume ndani akufokee na kuhisi huenda ulichepuka, na wengi wetu tulikuwa tukipigwa na hata baadhi ya ndoa zilivunjika, shida yote hii ilichangiwa na ukosefu wa maji, lakini kwa sasa tunaishukuru serikali kwa kutumalizia kero hii,” alieleza Juliana Simon.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Salawe, Emmanuel Maduhu alisema kupatikana kwa maji kutoka mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria kumepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama kwa wakazi wa kata ya Salawe.

“Kwa kweli kama jamii inavyoeleza, kupatikana kwa maji hayo kumepunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike walivyokuwa wakitendewa pindi wanapokwenda kutafuta maji, wengine walikuwa wakibakwa ama kupata vipigo wanapowakatalia wanaume kufanya nao tendo la ngono,” alieleza Maduhu.

Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Songambele kata ya Salawe wilayani Shinyanga (mwenye gauni la bluu) akijaza dodoso kuhusiana na uelewa wake juu ya masuala ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, anayeshuhudia ni mwenyekiti wake wa kitongoji, Ramadhani Masonoku. (Picha na Suleiman Abeid)