January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndoto ya kuzalisha mbolea kutosha nchini yatimia

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema lengo la Serikali la kuhakikisha mbolea ya kutosha inazalishwa nchini badala ya kutegemea kuagiza nje limetimia baada ya kiwanda cha mbolea cha Itracom kilichopo Nala jijini Dodoma kuanza uzalishaji.

Majaliwa alitoa kauli hiyo juzi baada ya kutembelea kiwanda hicho na kujionea shughuli za uzalishaji wa mbolea unaoendelea kiwandani hapo na hatua iliyofikiwa katika uwekezaji huo.

“ Rais Dkt. Samia amefurahi kusikia kiwanda hiki kimeanza uzalishaji.”

Alisema uwekezaji huo ambao unaenda sambamba na ujenzi wa viwanda vingine vitatu, kiwanda cha chokaa ya kilimo, vifungashio vya mbolea na kiwanda cha maziwa utaisadia Serikali katika kukabiliana na changamoto ya ajira.

“Kuna fursa nyingi katika kiwanda hiki ikiwemo upatikanaji wa mbolea ya uhakika na kwa gharama nafuu.”

Waziri Mkuu alisema eneo hilo la uwekezaji lazima liwe na huduma zote muhimu zinazohitajika ili kukiwezesha kiwanda hicho kuendelea na uzalishaji.

Huduma hizo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya uhakika ya barabara, maji, mawasiliano pamoja na nishati ya umeme. 

Vilevile, Majaliwa alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa Watanzania wanaofanyakazi kiwandani hapo kwamba wafanye kazi kwa weledi na uaminifu wa hali ya juu ili wawe mabalozi wazuri kwa wawekezaji wengine watakaokuja kuwekeza nchini. “Mkifanyakazi kwa bidii na uaminifu mtawarahisishia na wengine kupata kazi.”

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliipongeza na kuishukuru Serikali kwa juhudi kubwa ilizochukua za kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na hatimaye kumpata mwekezaji aliyejenga kiwanda hicho ambacho kinakwenda kuiwezesha nchi kupiga hatua kubwa katika suala zima la uzalishaji wa mbolea.

Pia, Waziri Bashe amewataka mawakala wanaotekeleza zoezi la usambazaji wa mbolea za ruzuku wafanye kazi hiyo kwa uaminifu kwa kuwa Serikali ipo makini na itahakikisha inaendelea kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kufanya udanganyifu.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho, Nduwimana Nazaire alisema ujenzi ulianza Julai 2021 na kimeanza uzalishaji wa tani 200,000 na kimeajiri watu 972.

“Mitambo ya laini ya pili na ya tatu imeshafika na ujenzi unaendelea na mwakani tutakuwa tumekamilisha ujenzi wa mitambo itakayozalisha tani milioni moja kwa mwaka.”

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa uongozi wa kiwanda hicho umejipanga kuhakikisha wanazalisha mbolea zenye ubora wa viwango vya juu na rafiki kwa udongo na mazingira ya eneo husika lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini na hivyo kuwaongezea tija wakulima.