January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakazi Tabora waaswa kulinda vyanzo vya maji

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian amewataka wakazi wa Mkoa kuacha kulima kando kando ya vyanzo vya maji ili kuepusha vyanzo hivyo kukauka.

Ametoa rai hiyo hivi karibuni alipokuwa akiongea na wakazi ya Kijiji cha Kigombe, Kata ya Kabila katika halmashauri ya manispaa Tabora alipokuwa katika ziara ya kutembelea Bwawa la Maji la Igombe.

Alisema bwawa hilo ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya maji katika Mkoa huo ambavyo vimekuwa vikiharibiwa kwa kutokana na shughuli za kibinadamu zinazofanyika.

Alisema uharibifu wa mazingira unaoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali hupelekea kuwepo ukame katika maeneo hayo hivyo kupelekea kukosa mvua za kutosha na maji kupungua katika mabwawa.

Alitaja athari zake kuwa ni kupungua kwa uzalishaji wa nishati ya umeme katika mabwawa mengi nchini husababishwa na kuathiri upatikanaji wa huduma hiyo.

RC Batilda alisisitiza kuwa kama jamii itazingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi na kufuata maelekezo ya wataalamu tutaepuka athari hizo na kuongeza kuwa hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa kwa wote wanaoenda kinyume.

‘Hatutakubali vitendo hivi viendelee, tumeanza kampeni ya kupanda miti katika vyanzo vyote vya maji na kuanzia sasa tutasimamia kikamilifu sheria zilizopo ili kurejesha mazingira ya vyanzo hivyo katika hali yake ya kawaida’, alisema.

Aidha katika kuhakikisha vyanzo vyote vya maji katika Mkoa huo vinakuwa salama, RC aliagiza Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Mkoani humo kubainisha maeneo yote yenye vyanzo vya maji ili ipandwe miti ya kutosha.

Ili zoezi hilo kuwa endelevu, aliagiza Wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanapanda miti mil 1.5 ambapo zaidi ya miti mil 12 inatarajiwa kupandwa na halmashauri zote 8 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais.

Meneja wa TFS Kanda ya Magharibi Ebrantino Migiye alimshukuru kwa kukubali kuzindua kampeni hiyo na kumhakikishia kuwa wameotesha miche ya miti aina mbalimbali ya kutosha ambayo itapandwa katika maeneo yote ya vyanzo vya maji.

Aliitaka jamii kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita katika suala zima la utunzaji wa mazingira ili kuepusha athari za ukosefu wa mvua na kulinda mazingira yao.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian akiwa katika picha ya pamoja na wananchi na kikosi kazi kilichoshiriki zoezi la upandaji miti 500 katika Kijiji cha Kigombe, Kata ya Kabila katika manispaa Tabora ili kulinda chanzo cha bwawa la maji la Igombe. Picha na Allan Vicent