January 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana watakiwa kutumia ubunifu wao kuwa biashara

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Wabunifu kutoka shule mbalimbali za sekondari nchini wametakiwa kutumia ubunifu wao kuwa biashara ili kuongeza ajira nchini na kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii.

Hayo ameyasema Mkurugenzi wa huduma za Taasisi kutoka COSTECH, Emmanuel Mgonja wakati wa Hafla ya kufunga mafunzo kwaajili ya wabunifu ambao wameyapata kwa miezi kumi katika chuo kikuu cha Dar es salaam Desemba 15 mwaka huu Jijini Dar es Salaam.

“Mafunzo hayo ni muhimu ambayo yatachochea vijana wengi kuona kwamba sayansi ni fursa ambayo inaweza ikamsaidia mtu kupata biashara na kuongeza ajira kwa vijana na kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii”

“Wanasayansi wengi furaha yao ni kuona kile kitu walichokibuni kinatokea mara nyingi hawafikirii kuwa kitu hiko ni biashara kwa kuwepo kwenye mafunzo haya inawasaidia wanasayansi hao kubuni kitu na kuufanya ubunifu huo kuwa biashara” Alisema Mgonja.

Aidha Mgonja aliwaagiza waratibu wote wa mradi kutanua wigo wa kuongeza namba ya washiriki ili kuongeza hamasa kwa vijana hasa katika kupenda masomo ya sayansi na teknolojia.

“Wadau wote tufanye jitihada za kuwasaidia vijana hawa katika bunifu zao kuifanya sayansi iwe jambo la kibiashara na liweze kuwa na faida kwa taifa”

“Waratibu watanue wigo wa wanafunzi wanaoshiriki kutoka namba iliyopo kwenda namba ingine ili kutatua changamoto ambazo zipo kwenye jamii, kuongeza ajira kwa vijana na kuwajengea hamasa vijana katika kupenda masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabu” Aliongeza Mgonja.

Pia Mgonja aliwapongeza chuo kikuu cha dar es salaam kwa kuandaa mafunzo hayo, na washiriki wote ambao wamejitokeza kuonyesha bunifu zao.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Atamizi ya DTBi, Dkt. Erasto Mlyuka alisema kwenye programu hiyo wanakua na wataalamu wa kisayansi ambapo tunakua na walimu na wataalamu wa kibiashara

“Ushirikiano kati ya wataalamu wa kisayansi na kibiashara pamoja na atamizi ya DTBi inasaidia kukuza bunifu kufikia hatua ya kuingia sokoni “

Pia Dkt. Mlyuka alisema mpaka sasa wameshakua na bunifu zisizopungua 85 kwa shule 17 ambazo zimeshiriki ambapo Dar es Salaam shule 10 na Arusha shule 7 .

Dkt. Mlyuka alisema kutokana na matokeo mazuri yaliyoonekana kwa Dar es salaam na Arusha, kwa sasa wapo kwenye majadiliano ya kuhakikisha kwamba miradi huo uweze kuenea nchi nzima.

“Tumeugawa kwenye Kanda za nyanda za juu Kusini, kaskazini, Mashariki na Pwani, lakini pia tutafika na Zanzibar. Tupo kwenye hatua ya kuweza kuona tunaoanisha huu mpango wa kuendeleza sayansi, Teknolojia, ubunifu na hesabu kwa kuoanisha na programu ambayo ipo ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa kufanya hivyo tutakuwa na kitu ambacho ni endelevu”

Naye Meneja Mradi wa Feature uliyopo chini ya Tume ya Sayansi na Teknolojia kitengo cha Atamizi (DTBi), Joseline Sepeku alisema wanawasaidia wanafunzi hao kupata ujuzi zaidi pale wanapomaliza mafunzo yao ya awali kwa kuwapeleka katika kampuni ambazo zinaendana na kile kitu alichokibuni kuwapa mafunzo zaidi ili waweze kuelewa katika uhalisia.

“Mwaka jana tulikuwa na wanafunzi walioshinda kutoka shule ya Tambaza ambao walitengeneza kifaa kinachoendana na mfumo wa friji, waliweza kwenda kufanya mafunzo yao kwa muda wa wiki sita na kila kitu gharama ilikua juu yetu na wengine kutoka Arusha wakaenda safari ya Rai kwaajili ya kwenda kufanya mambo ya uchunguzi kwenye masuala ya kilimo”

Sepeku aliwataka wanafunzi kuthamini kile wanachofundishwa darasani ili kiweze kufanyika kuwa biashara katika bunifu zao .

Mwakilishi wa Rasi Ndaki ya Sayansi asilia na tumizi, Dkt. Kessy Kilulya aliwashukuru COSTECH kwa kuhakikisha kwamba mafunzo hayo yanaendelea kwa ufanisi kuhakikisha kwamba zinapatikana fedha za kuendeshea mafunzo hayo kila mwaka ambapo kumekua na mafanikio makubwa kwa maana ya kwamba kumekua na maboresho makubwa.

“Tuendelee kutanua wigo, tulianza na shule chache na sasa tupo shule 10 washiriki wakiwa watano, pengine kwasababu inajenga fursa kwa vijana wengi, hivyo tujitahidi kupata shule nyingi na washiriki wengi kwa kila shule itakayoshiriki”