Na Mwandishi Wetu, TimesMajiraonline,Dodoma
RAIS wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameandika rekodi kwa kuwa mwanamke wa kwanza kutoka vyama vikongwe barani Afrika kuchaguliwa kwa kishindo kwa kura nyingi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais Dkt. Samia amechaguliwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika jana (Des 7) kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma kwa kupata kura 1,914 kati ya kura 1,915 zilizopigwa, ambapo kura moja ilimkataa.
Katika kinyang’anyiro hicho, Dkt. Samia alikuwa mgombea pekee baada ya juzi Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kupitisha jina lake kuwania nafasi hiyo kwa mwaka 2022 hadi 2027.
Mwenyekiti wa Muda ambaye ni Rais Mstaafu wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein ndiye alitangaza ushindi wa Dkt. Samia.
Kwa ushindi huo, Dkt. Samia ameandika rekodi ya kwanza nchini na Afrika kwa ujumla kuwa mwenyekiti wa kwanza wa chama kikongwe kuchaguliwa kwa kura kushika wadhifa huo.
Dkt. Samia amekuwa Mwenyekiti wa CCM tangu Aprili Mosi, 2021 kufuatia kifo cha Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dkt. John Magufuli.
Hiyo ni rekodi ya pili kuandikwa na Dkt. Samia baada ya Machi 19, mwaka jana kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo nchini.
Dkt. Samia anakuwa Mwenyekiti wa CCM wa sita, ambapo watangulizi wake wote walikuwa wanaume. Wenyeviti wa CCM Taifa waliomtangulia Dkt. Samia ni pamoja na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwenyi, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa.
Wengine ni Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Magufuli.
Kwa upande wa matokeo ya kura kwa Nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Dkt. Shein alimtangaza Komredi Abdulrahman Kinana mshindi ambaye aliibuka kwa kura 1,913, kati ya kura zote 1,915 zilizopigwa, ambapo kura mbili ziliharibika
Katika kinyang’anyiro hicho kinana hakuwa na mpinzani kama ilivyokuwa kwa Dkt. Samia. Kabla ya uchaguzi huo kinana alikuwa akishikilia nafasi hiyo ya Makamu wa Mwenyekiti wa CCM.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Shein alimtangaza Dkt. Hussein Ally Mwinyi kuwa mshindi kwa kupata kura 1,912, huku kura tatu zikimkataa.
Nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya s
Saba wa Zanzibar ,Dkt. Shein ambaye amemaliza muda wake.
Katika nafasi 20 za Halmashauri Kuu (NEC) Bara, mawaziri walioomba nafasi hiyo wengi wamepata ambao ni Waziri wa Nishati January Makamba, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba, na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt. Ashatu Kijaji. Waziri wa Katiba na Sheria George Simbachawene amepigwa chini.
More Stories
Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia