November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madaktari bigwa kutoka Bugando na Sekou-Toure waungana kutoa huduma za afya ikiwemo sikoseli

Na Judith Ferdinand, Times Majira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa magonjwa ambayo yanaongoza kupokelewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure iliopo mkoani hapa ni wagonjwa wa sikoseli.

Huku takwimu zinaeleza kuwa zaidi ya watoto 11, 000 huzaliwa na vinasaba vya ugonjwa wa sikoseli kwa mwaka ambapo asilimia 7 ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano hutokana na ugonjwa huo.

Hivyo timu ya madaktari bingwa 20 kutoka hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando na Sekou-Toure wameweka kambi ya siku tano katika hospitali ya Sekouture kwa ajili ya kutoa huduma za afya ikiwemo ugonjwa wa sikoseli.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo,Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Sikoseli Dkt.Gloria Mapunda, ameeleza kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa wanaoripotiwa katika hospitali hiyo ni wa sikoseli na kueleza kuwa ugonjwa huo unazuilika iwapo wagonjwa watatibiwa kwa wakati.

Amesema takwimu zinaeleza kuwa zaidi ya watoto 11, 000 huzaliwa na vinasaba vya ugonjwa wa sikoseli kwa mwaka huku asilimia 7 ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano hutokana na ugonjwa huo.

Hata hivyo amewatoa hofu wananchi kuwa vipimo vya ugonjwa huo vinapatikana na iwapo mgonjwa atabainika na ugonjwa huo atapatiwa matibabu yatakayosaidia kupunguza maumivu ya mifupa.

Akizungumzia kambi hiyo Mganga Mfawadhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou-Toure Dk. Bahati Msaki, ameeleza kuwa wameamua kuweka kambi hiyo ili wananchi waweze kuchunguza afya zao mapema na kupata matibabu kabla ya madhara hayajawa makubwa.

Dkt Bahati ameeleza kuwa katika kambi hiyo kutakuwa na vipimo vya sikoseli,moyo sukari, ugonjwa wa tumbo na saratani ya damu, CT-Scan, Xray na Eco pamoja na huduma za kibingwa.Pia ameeleza kuwa kutakuwa na huduma za kibingwa za macho, miozi, watoto,meno, magonjwa ya akina mama na uzazi, magonjwa ya mfumo wa damu na chakula, akili, kusafisha damu pamoja na maabara za dawa.

Akizindua Lambi hiyo Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Elikana Baladya amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya kwani ni muhimu kuwa na afya njema.

Naye mmoja wa wananchi waliofika kwenye vipimo hivyo,akiwemo Mariam Idd ameipongeza serikali kwa maamuzi ya kusogeza huduma hizo za kibingwa na kuomba ziwe endelevu.

“Usiwe mwanzo wa huduma hizi zije mara kwa mara ili kuwasaidia wananchi kuchunguza afya zao lakini pia huduma hizi zipelekwe vijijini kwakuwa kuna wananchi wanashida na hawana uwezo wa kufika kwa ajili ya matibabu,” amesema Mariam.

Ibrahim Lyimo amesema huduma hiyo ni nzuri na inapatikana kwa nadra na kuwaomba wataalam wa afya kuitoa mara kwa mara.

Wanachi wakiendelea kupatiwa matibabu na madaktari bingwa walioweka kambi katika hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou- Toure.
Mmoja wa madaktari bigwa akiendelea kutoa huduma kwa mwananchi aliyejitokeza kupata huduma ya afya waliojitokeza kwenye kambi ya siku tano ya madaktari bigwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure.