October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro,Juma Ngwisu akimtembeza katika mazingira ya Soko Kuu la Morogoro mjini Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania leo. (Picha na Sauti ya Uponyaji).

Nabii Joshua aipongeza Serikali kwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Morogoro

KIONGOZI Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli kwa kushirikiana na wasaidizi wake kutokana na kazi kubwa za maendeleo wanazozifanya kwa Watanzania wote.

“Utekelezaji wa miradi inayofanyika ndani ya Taifa letu imekuwa ya baraka sana, baada ya kutembelea ujenzi wa Soko Kuu hapa Morogoro Mjini, nimebaki nikimwambia Yesu asante kwa kutupa viongozi sahihi, soko hili ni mfano tosha wa miradi mingi ya maajabu kwa taifa letu, Mungu awabariki viongozi wetu chini ya Rais Dkt.John Magufuli kwa kazi nzuri, hakika Watanzania tunaelekea pazuri;

Nabii Joshua ameyasema hayo mjini Morogoro baada ya kufanya ziara katika soko hilo kwa ajili ya kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ikiwemo kuifanyia maombi maalum ili Mungu aweze kuiongoza katika hatua zote za utekelezaji.

Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala (kushoto) akimpongeza Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro,Juma Ngwisu kwa kazi nzuri ya usimamizi wa Soko Kuu la Morogoro na miradi mingine. (Picha na Sauti ya Uponyaji).

Pia Kiongozi huyo alimpongeza Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro,Juma Ngwisu kutokana na uchapa kazi ambao umewezesha mradi huo wa soko kuwa wa mfano mjini hapa.

Amesema, ili Rais Magufuli aweze kufanikisha ahadi zake kwa wananchi kwa wakati, viongozi wa chini wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuisimamia miradi yote inayotekelezwa ikiwemo kuzingatia kuweka hofu ya Mungu mbele, kwa kuwa penye Mungu mambo huwa yanafanyika kwa ufanisi.

“Nichukue nafasi hii kukupongeza sana ndugu Injinia (Mhandisi) wa Manispaa ya Morogoro kwa kazi nzuri, hakika kazi hii imeendelea kuupa mji wetu hadhi kubwa, Mungu akubariki sana,”amesema Nabii Joshua.

Muonekano wa Soko Kuu la Morogoro ambalo limejengwa kisasa. (Picha na Sauti ya Uponyaji)

Aidha, Nabii Joshua alitumia muda huo kufanya maombi maalum na kumweleza Mungu kuwa msimamizi mkuu wa miradi yote inayotekelezwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ili iweze kukamilika kwa wakati.

Amesema, Serikali imekuwa mstari wa mbele kutekeleza miradi mbalimbali kuanzia nishati, afya, elimu, masoko, maji, miundombinu ya reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege na mingine mingi ambayo inataka fedha nyingi,na imekuwa ikipitia vikwazo vingi, lakini kwa msaada wa Mungu imepiga hatua tena kwa fedha za ndani.

Nabii Joshua pia ametumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania na watumishi wa Mungu kuendelea kuliombea Taifakila saa kwani, Mungu amezidi kuwa mwingi wa rehema kwa Tanzania.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro,Juma Ngwisu amewapongeza watumishi wa Mungu kwa kuendelea kuliombea Taifa,kwani maombi yao yamekuwa msingi wa mafanikio katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema, Serikali inatambua mchango wao wa kuendelea kuwajenga kiroho Watanzania, jambo ambalo limewezesha ustawi bora wa kimaadili na malezi katika jamii zetu.