November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali imeombwa kuwawajibisha wanaomba rushwa ya ngono kwa wanafunzi na wafanyakazi

Na Penina Malundo 

DUNIA ikiwa  inafanya maadhimisho ya Siku 16 kupinga ukatili wa jinsia,  Chama  cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na wanamtandao wa kupinga ukatili wa jinsia  hapa nchini pamoja na  wadau wa maendeleo,wameendelea kuiomba serikali kuendelea kuwawajibisha wale wanaomba rushwa ya ngono kwa wanafunzi na kwa wafanyakazi ili kuweza kupiga vita vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia.

Akitoa tamko la siku 16 kupinga ukatili wa kijinsi,Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA,Dkt.Rose  Reuben wakati akiongea na wa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,amesema TAMWA  ilitekeleza mradi mwingine uliofanana na huu,kwa kufanya utafiti kuangalia hali halisi yabrushwa ya ngono katika vyumba vya habari.

Amesema TAMWA katika  tafiti zake kuna tatizo kubwa la rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono mahala pa kazi na katika elimu ya vyuo vikuu.”Tamwa na wadau wengine tunajisikia fahari  kuwa sehemu ya kuibua mengi kuhusu athari ya rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono mahali pa kazi na katika taasisi za elimu na kwa kuendeleza mjadala huo katika jamii kupitia vyombo vya habari, “amesema

Amesema pia  rushwa ya ngono katika vyuo vikuu ni janga kubwa linalochagiza kushuka kwa kiwango cha taaluma,kuzalisha wahitimu wasiona sifa  na kuharibu talantabkwa wale wanaokataa rushwa hiyo.”Mbali na wasomi kuna changamoto kubwa Wanahabari wengi kuacha kazi kwa kuhofia udhalilishaji wa kijinsia katika tasnia hiyo,wapo wanafunzi walioacha vyuo na kuacha shule kwa kuombwa rushwa ya ngono,”alisema 

Aidha Dkt.Rose amesema Juzi akifungua kongamano la wadau wa rushwa ya ngono kwa wanafunzi na wakufunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma Naibu Waziri wa Utumishi Deogratius Ndejembi,alisena rushwa ya ngono inasababisha kuzalishwa wasomi wasio na tija na kuwanyima haki wanafunzi.

Amesema  TAMWA kupitia miradi yake inayohimiza kuzuia ukatili katika jamii, tumeweza kufanya yafuatayo;

Kwanza, kuvunja ukimya uliotawala miongoni mwa wanahabari katika kusema kinagaubaga au kundika kuhusu madhila wanayopitia wanapodhalilishwa kingono.

“TAMWA imebaini asilimia 48 tu ya wanahabari ndio wanaoweza kusema wazi kuhusu madhila ya rushwa ya ngono wanayopitia katika vyumba vya habari. Asilimia 52 inayobaki, hawawezi kusema wazi kuhusu changamoto hiyo,”amesena 

Amesema katika tafiti hizo zinabaini kuwa wanahabari wengi wanawake wameacha kazi kwa kuhofia udhalilishaji wa kijinsia katika tasnia hiyo, wapo wanafunzi waliohama vyuo na kuacha shule kwa kuombwa rushwa ya ngono.  

Naye  Dk Kantanta Simwanza kutoka Taasisi ya MenEngange Coalition, amesema imefika wakati wa Serikali kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza vitendo vya ukatili na unyanyasaji. 

Amesema rushwa ya ngono imezuia wanawake wengi kufikia ndoto zao, hivyo ni jukumu la kila mmoja kupaza sauti kukemea vitendo hivyo. 

“Wanaume ndo tunatajwa sana kama wahusika wakuu wa vitendo hivi…hivyo tunaungana na jamii kuvikemea na kukumbushana kuwa wajibu wetu ni kukagua vyeti sio maungo ya mtu.

“Pamoja na hayo tunaiomba serikali iridhie mkataba huo ili kuondoa changamoto hiyo kwani rushwa ya ngono imezuia wanawake kufikia ndoto zao,” alisema Dk. Simwanza. 

Mratibu Kitaifa wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WILDAF),Wakili Msomi Anna Kulaya, amesema wanatamani kuona Tanzania hakuna vitendo vya ukatili wa kijinsia, rushwa ya ngono pamoja na ndoa za utotoni. 

Hata hivyo alisema pamoja na kuwepo kwa muongozo wa kuwekwa kwa madawati ya kijinsia vyuoni bado muitikio umekuwa mdogo.

“Tangu ulipozinduliwa muongozo huu Novemba 25, mwaka jana lakini mpaka sasa yapo madawati 20 tu kwa nchi nzima. Nitoe wito kwa vyuo vingine vikuu na vya kati kufungua haya madawati ambayo yatasaidia kunusuru mabinti wetu,” amesema Kulaya.