Na Martha Fatael, TimesMajira Online, Moshi
MAMLAKA ya mapato nchini (TRA) mkoani Kilimanjaro, imevuka malengo ya ukusanyaji mapato kwa kipindi Cha mwaka 2021/2022 kwa kukusanya Sh Bil 227 kati ya makadirio ya Sh Bil 210 kwa kipindi hicho.
Makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 108 ambayo ni mafanikio makubwa baada ya wafanyabiashara kuelewa umuhimu wa ulipaji kodi.
Meneja wa TRA mkoani hapa, Masawa Massatu amesema hayo katika taarifa yake kwenye wiki ya shukrani kwa mlipa kodi na kwamba kupitia kodi serikali imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo madarasa, hospitali, zahanati na miradi mingine ya maendeleo.
Massatu ametaka wafanyabiashara Mkoani humo kujitokeza kupatiwa elimu ya masuala ya kodi ili kuepukana na changamoto za kikodi ambazo wamekuwa wakikumbana nazo.
“Tofauti na mwaka uliopita wa 2020/2021 tulipata ongezeko la bill 33 sawa na asilimia 17” amesema
Mapema Mkuu wa wilaya ya Moshi, Abas Kayanda ametaka wafanyabiashara kuona suala la ulipaji kodi ni jukumu lao kama sehemu ya kuchangia maendeleo ya Taifa.
Kayanda amewataka wafanyabiashara kuitumia wiki ya mlipa Kodi kupata uelewa kupitia elimu itakayokuwa ikitolewa kwani itawasaidia kukukua kibiashara kwa kulipa Kodi inayotakiwa badala ya kukumbana na faini mbalimbali.
Katika hatua nyingine ameitaka mamlaka ya mapato Tanzania TRA Mkoa wa Kilimanjaro kukusanya Kodi Kwa kutotumia nguvu kama serikali ambavyo imekuwa ikisisitiza.
Hata hivyo kauli mbiu katika wiki ya shukrani kwa mlipa Kodi ni ahsante Kwa kulipa Kodi Kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya nchi yetu.
More Stories
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi
SACP Katabazi: Elimu ya usafirishaji wa kemikali bado ni muhimu kwa watanzania