Na David John
Mbunge wa Mbagala Wilayani Temeke Abdalah Chaurembo amewashauri viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tawi la Kiponza Kata ya Chamazi kushirikiana na viongozi wa serikali ya Mtaa wa Kiponza kutafuta eneo la gharama nafuu kwa ajili ya kujenga ofisi ya chama.
Chaurembo ametoa ushauri huo hivi karibuni katika mkutano wa wanachama wa CCM tawi la Kiponza Kata ya Chamazi jimbo la Mbagala, uliofanyika sambamba na kuwashukuru wananchi wa mtaa huo kwa kuendelea kukiamini chama cha mapinduzi nakukipatia ridhaa ya kuongoza.
Amesema kuwa CCM tawi la Kiponza haina ofisi ya chama hali ambayo imepelekea kumuomba yeye kama mbunge kuwasaidia kupata fedha kiasi cha shilingi milioni 14 kwa ajili ya kulipia eneo walilolipata ili wajenge ofisi ya kisasa hata hivyo Mbunge Chaurembo amewashauri kutafuta eneo la muda lenye gharama nafuu ili wajenge ofisi hiyo huku wakiendelea kutafuta fedha ya kununua eneo jingine kubwa la kujenga ofisi ya kudumu.
“Ndugu zangu nimesikia kwenye risala yenu mnataka milioni 14 kwa ajili ya kujenga ofisi ya kisasa tawi la Kiponza,naomba niwashauri mtafute eneo lenye gharama nafuu mtakaloweza kujenga ofisi nzuri itakayotumika kwa muda,hapa kuna eneo la Songas mnaweza kuwaomba wawapatie eneo mjenge ofisi huku nanyinyi mkilinda eneo lao” amesema chaurembo.
Awali akisoma risala Katibu wa Chama Cha Mapinduzi tawi la Kiponza Msosea Moshi amesema kuwa tawi hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa ofisi ya CCM tawi la Kiponza pamoja na shule ya msingi na sekondari hali inayopelekea msongamano wa watoto katika shule ya Mbande na Fufu.
Amesema kuwa Viongozi wa CCM tawi la Kiponza kata ya Chamazi wamefanya mpango wa kutafuta eneo la chama kwa ajili ya kujenga ofisi baada ya eneo la awali lililokua na mgogoro kushindwa kesi hivyo eneo lililopatikana lina thamani ya shilingi milioni kumi na nne nakwamba lipo kando ya eneo la Songas ambapo pia lina kisima cha maji.
“Wewe pamoja na wanachama wa tawi la Kiponza viongozi wa kata ,wilaya tunaomba tushirikiane kulilipia eneo hili,tunakuomba sana utusaidie kwa hali na mali kututafutia wadau wengine Mheshimiwa mbunge ili tujenge ofisi ya chama yenye hadhi ya tawi la Kiponza ambalo lina muda mrefu sana” alisema Msosea kupitia risala hiyo.
Nae Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi tawi la Kiponza Amina Puga amesema kuwa viongozi wa CCM tawi la Kiponza watandelea kua imara katika kuwaletea wananchi maendeleo kwani wananchi hao bado wana imani na chama hicho.
Aidha, Amina ametumia fursa hiyo kuwashukuru wanachama wa CCM tawi la kiponza kwa kuwachagua huku akisisitiza kushirikiana na viongozi wa serikali ya mtaa wa kiponza katika kutekeleza Ilani ya Chama hicho kwa vitendo na kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kuwaletea maendeleo wananchi.
More Stories
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi
SACP Katabazi: Elimu ya usafirishaji wa kemikali bado ni muhimu kwa watanzania