November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yashauriwa kuepuka msongo wa mawazo,kupambana na ugonjwa wa kisukari

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Jamii imeshauriwa kuishi maisha kulingana na uwezo walio nao ili kuepuka msongo wa mawazo ambao uchangia kupata ugonjwa wa kisukari sanjari na kupata muda wa kutosha kupumzika.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha ugonjwa wa Kisukari Tanzania Profesa Andrew Swai,katika maadhimisho ya siku ya ugonjwa wa kisukari duniani ambayo uadhimishwa kila mwaka ifikapo Novemba 14, ambapo nchini hapa kitaifa wameadhimisha Novemba 13,2022 wilayani Misungwi.

Ambapo maadhimisho hayo yameandaliwa na Chama cha ugonjwa wa kisukari Tanzania kwa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Shirikisho la Vyama vya magonjwa yasiyoambukiza Tanzania.

Profesa Swai, ameeleza kuwa watu wanapaswa kuishi maisha kulingana na kipato chao ili kuepuka ugonjwa wa kisukari huku alitumia msemo wa “usiige kujisaidia kwa tembo,utapasuka msamba”.

Mbali na hayo pia wazingatie muda wa kupumzika kwa kuhakikisha wanapata usingizi wa kutosha ili mwili uweze kusawazisha palipo haribika kwani binadamu matengenezo ya mwili yanafanyika usiku ukiwa umelala.Pia ameushauri jamii kuacha matumizi ya kiwango cha juu cha sukari na chumvi ambapo ameeleza kuwa kwa siku mtu anapaswa kutumia vijiko vitano vya sukari na kijiko kimoja cha chumvi.

Ameeleza kuwa awali katika utafiti ulionesha kuwa kati ya watu 100 asilimia 1, wakigundulika na kisukari lakini mwaka 2012 utafiti unaonesha wagonjwa wameongezeka kutoka asilimia 1 na sasa ni asilimia 9.

“Kati ya watu 100,watu 9 wanaugua kisukari ni tatizo kubwa,tunahitaji kuzuia haya magonjwa kwani tiba yake ni gharama kubwa lakini yanaweza kuzuilika kwa kufuata mtindo bora wa maisha,kula mlo kamili na kutoongeza sukari kwenye chakula na vinywaji,usizidishe vijiko vitano kwa siku na usitumie zaidi ya kijiko kimoja cha chumvi kwa siku,”ameeleza Prof.Swai.

Mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza Wilaya ya Misungwi Daktari Chausiku Kasala, ameeleza kuwa kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2021 kupitia Idara ya Afya Halmashauri ya Wilaya hiyo ina jumla ya wagonjwa wa 586 wenye tatizo la kisukari ambao walipima,kusajiliwa na kuthibitika kupitia mfumo wa kutolea taarifa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa mpango wa taifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza,Valeria Millinga, ameeleza kuwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari uchangia asilimia 33 ya vifo nchini hapa.

“Asilimia 9.1 ya watanzania wana ugonjwa wa kisukari na katika nchi 10 barani Afrika kwa magonjwa ya kisukari Tanzania inashika nafasi ya 8 hivyo utaona kwa kiasi gani nchi yetu ilivyoathirika na ugonjwa huu,”ameeleza Valeria.

Ameeleza kuwa serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, ambapo katika maadhimishonya wiki ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo mwaka huu kitaifa yamefanyika mkoani Mwanza ambapo takribani wananchi 3000 wameweza kupata huduma na kati yao takribani 34 wamegundulika kuwa na viashiria vya ugonjwa wa kisukari.

Naye Mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt.Bakari Salum, ameeleza kuwa wataendelea kusimamia Halmashauri kwa kuhakikisha vituo vya afya vinatoa huduma kwa mujibu wa wananchi wananvyokuwa wanahitaji huduma ya afya.

“Hivi karibuni tutakuwa na mafunzo Mkoa wa Mwanza na Misungwi ikiwemo kwa watumishi wa afya ili baada ya mafunzo hayo kila kituo cha afya kitakachopata mafunzo haya kitatakiwa kianzishe kliniki ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari na sisi kama TAMISEMI tutalisimamia hilo,”ameeleza Dkt.Salum.

Mwenyekiti wa Chama cha ugonjwa wa Kisukari Tanzania Profesa Andrew Swai, akizungumza katika maadhimisho ya siku ya ugonjwa wa kisukari duniani ambayo uadhimishwa kila mwaka ifikapo Novemba 14, ambapo nchini hapa kitaifa wameadhimisha Novemba 13,2022 wilayani Misungwi.
Mmoja wa mwananchi akipimwa na mtoa huduma ya afya katika maadhimisho ya siku ya ugonjwa wa kisukari duniani ambayo uadhimishwa kila mwaka ifikapo Novemba 14, ambapo nchini hapa kitaifa wameadhimisha Novemba 13,2022 wilayani Misungwi.
Wanafunzi was shule ya sekondari ya wasichana Misungwi wakiandamana kuelekea uwanjani yalikonfanyika maadhimisho ya siku ya ugonjwa wa kisukari duniani ambayo uadhimishwa kila mwaka ifikapo Novemba 14, ambapo nchini hapa kitaifa wameadhimisha Novemba 13,2022 wilayani Misungwi.