November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Usawa wa kijinsia kuangaliwa kwa jicho la karibu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum Dkt Zainab Chaula akifungua mafunzo ya Masuala ya Usawa wa Kinjisia kwa Wakurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara mbalimbali Tanzania Bara jijini Dodoma Novemba 10, 2022.

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo Ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amesema Serikali imeendelea kuweka jitihada mbalimbali zitakazoleta usawa wa kijinsia katika jamii kwa uharaka zaidi.

Dkt. Chaula ameyasema hayo katika kikao Kazi kilichojumuisha Wakurugenzi wa Sera na Mipango na Waratibu wa Dawati la Kijinsia wa Wizara za Kisekta Jijini Dodoma, Novemba 10, 2022.

Dkt. Chaula amesema Tanzania imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza Ajenda ya Usawa kwa kuwepo na Katiba ya Nchi inayosema binadamu wote ni sawa na kuundwa kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum kusimamia utelezwaji wa Usawa na Uwezeshaji wa Uchumi kwa kuzingatia Usawa wa Kijinsia.

“Ili tuweze kutimiza adhma ya Usawa wa kijinsia nchini, Serikali imeendelea kuweka jitihada zake katika kubainisha Mikakati na kutoa mafunzo ya Jinsia katika ngazi mbalimbalia za utendaji ili kurahisisha usawa wa Kijinsia kwa kuzingatia Sera ya Maendeleo ya Wanawake ya Jinsia ya Mwaka 2000 na mkakati wake wa Utekelezaji”amesema Dkt. Chaula.

Aidha Dkt. Chaula amesema ili kuhakikisha masuala ya Usawa yanaingizwa kwenye Sera, Mikakati na Programu za Sekta husika Serikali iliunda Dawati la Jinsia katika ngazi ya Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea,Taasisi,Mikoa na Wilaya ili kuweza kuratibu utekelezaji wake.

“Dawati la Jinsia lina jukumu la kuratibu masuala ya Kijinsia na kuhakikisha masuala hayo yanaingizwa kwenye Sera, Mipango na Programu za Sekta husika Ili kuwepo na Watendaji wenye ujuzi, uzoefu na stadi zinazotakiwa za Masuala ya Kijinsia, Wizara imejiwekea Utaratibu wa kutoa mafunzo kwa Watendaji wa Dawati hilo katika ngazi zote.” alisema Dkt Chaula

Aliongeza kwamba utoaji wa mafunzo hayo kwa Wakurugenzi wa Sera na Mipango ni kwa ajili ya kuleta uelewa kwa uwiano ulio bora zaidi na hatimaye kuleta msisitizo wa uingizaji wa Masuala ya Jinsia katika Sera,Mipango na Bajeti za Wizara na Taasisi hizo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Grace Mwangwa amesema Wizara kwa sasa ipo katika mchakato wa kuhuisha Sera ya Maendeleo ya Wanawake ya Jinsia ya Mwaka 2000 ambayo itaendelea kutoa Mwanga kwa namna gani masuala ya Usawa wa Kijinsia yasimamiwe na kuratibiwa vyema katika Wizara na Taasisi za Serikali ili ziwe mfano katika harakati za Usawa wa Kijinsia nchini.

Nao baadhi ya Washiriki wa mafunzo hayo wamesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambao utasaidia kujipanga na kujiweka sawa zaidi katika kuhakikisha masuala ya Usawa wa Kijinsia yanapewa kipaumbele katika Wizara na Taasisi za Serikali hasa kwa kutengewa Bajeti na kutekelezwa kama mikakati na Miongozo inavyosema.

Baadhi ya Washiriki katika mafunzo ya Masuala ya Usawa wa Kinjisia kwa Wakurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara mbalimbali Tanzania Bara wakifuatilia mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dodoma Novemba 10, 2022.