Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 imefanikiwa kukusanya kiasi cha zaidi ya bilioni 5 (5,016,854,151.61).
Akisoma taarifa katika kikao cha Baraza la Madiwani,kwa kipindi cha robo ya kwanza Julai-Septemba mwaka huu kilichofanyika leo Novemba 11,2022,katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary,ameeleza kuwa makusanyo hayo ni sawa na asilimia 37.1 ya makisio ya bajeti ya mwaka 2022/2023 ambayo ni mapato ya ndani.
“Kwa mwaka wa fedha uliopita tulikuwa na lengo la kukusanya kiasi cha milioni 850 kwa mwezi,mwaka huu tumepiga hatua twenakwenda kukusanya zaidi ya bilioni 1 kila mwezi na uhalisia tumekusanya asilimia 25 na asilimia zilizoongezeka kufikia asilimia 37 imechangiwa na mradi wetu wa viwanja,”ameeleza Mhandisi Apolinary.
Sanjari na hayo Mhandisi Apolinary, ameeleza kuwa katika robo hiyo zaidi ya milioni 890 fedha za mapato ya ndani walizielekeza katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwa Kata zilizopo kwenye halmashauri hiyo katika sekta ya elimu, ujenzi,afya, maendeleo ya jamii na ardhi.
Sekta ya Ujenzi.
Ameeleza kuwa katika sekta ya ujenzi umaliziaji wa jengo la utwala kiasi cha zaidi ya milioni 123,mradi wa matofali zaidi ya milioni 65,kuwezesha uwekaji wa umeme kwenye soko la muda la Magomeni zaidi ya mIlioni 3 na kuwezesha matengenezo ya barabara ya mtaa wa Bwiru Ziwani kiasi cha milioni 7.
Sekta ya elimu.
Katika sekta ya elimu,
Ununuzi wa madawati katika shule ya msingi kiasi cha zaidi ya milioni 34, ujenzi wa vyumba vya madarasa shule ya msingi Kangaye milioni 54, ujenzi wa matundu ya vyoo 20 shule ya msingi Lukobe milioni 20 na ukamilishaji wa darasa shule ya msingi Kiloleli milioni 12.5.
Huku upande wa elimu sekondari
Utengenezaji wa vitanda shule ya wavulana Bwiru kiasi cha milioni 7.5, ukamilishaji wa ujenzi wa bweni la shule ya sekondari ya wavulana Bwiru milioni 58, ujenzi wa matundu ya vyoo shule ya sekondari Bujigwa zaidi ya milioni 4.
“Tumefanikiwa kukamilisha ujenzi wa maboma 45,ofisi 4 na matundu ya vyoo 4,katika baadhi ya shule za msingi,hii ni kuwapongeza wananchi na viongozi katika maeneo haya kwa jitihada walizofanya,” Mhandisi Apolinary Sekta ya afya.
Mhandisi Apolinary, ameeleza kuwa katika robo hiyo wamefanya ujenzi wa zahanati Kata ya Kawekamo kiasi cha milioni 50, ujenzi wa wodi ya kina mama kituo cha afya Buzuruga.milioni 50.
Sekta ya Maendeleo ya Jamii.
Ameeleza kuwa wamewezesha mfuko wa wanawake,vijana na walemavu kwa kiasi cha zaidi ya milioni 194.
Sekta ya Ardhi.
Aidha ameeleza kuwa kwa upande wa ardhi kiasi cha zaidi ya milioni 204 kwa ajili ya fidia ya Ardhi katika maeneo ya shule ya sekondari Nyasaka na Lumala.
Kwa upande wa Madiwani wa Halmashauri hiyo wamempongeza Mkurugenzi kwa kufanikisha mambo mbalimbali ikiwemo ukusanyaji huo wa mapato pamoja na kutoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali.
Diwani wa Kata ya Pasiansi Rosemary Mayunga,amepongeza Mkurugenzi huyo kutoa fedha kwa ajili ya kununua vitanda na ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari ya wavulana Bwiru pamoja na utengenezaji wa barabara kwa wananchi wa mtaa wa Bwiru Ziwani ambao awali walikuwa wanapita katikati ya shule ya wavulana Bwiru.
“Kitu ambacho kimewagusa sana wananchi wa Kata ya Pasiansi ni hii barabara ya mtaa wa Bwiru Ziwani,historia kwao kwa miaka mingi tangu kuzaliwa kwa Kata hii wameangaika sana walikuwa wanapita katikati ya shule ya sekondari ya wavulana Bwiru hali ilikuwa inahatarisha usalama wa wanafunzi,”ameeleza Rosemary.
Diwani wa Kata ya Kahama Samweli Mwita,ametoa pongezi kufuatia ujenzi wa matundu ya vyoo 20 katika shule ya msingi Lukobe,kwani imewasaidia wanafunzi wa shule hiyo ambao awali walilazimika kwenda shule jirani kujisaidia.
Ambapo hali hiyo ilikuwa ni changamoto sana hasa wakati wa mapumzuko saa nne utakutana na msururu wa wanafunzi wakiwa wamepanga mstari kwa ajili ya kwenda kujisaidia kama vile watu wanaenda kuchukua chakula.
More Stories
Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia