Na Ashura Jumapili, TimesMajira Online, Bukoba,
Majeruhi 23 kati ya 24 wa ajali ya ndege ya Kampuni ya Precision waliokuwa wakitibiwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Kagera wameruhusiwa na mmoja bado anaendelea kupatiwa matibabu.
Kauli hiyo imetolewa na msemaji wa Serikali Gerson Msigwa wakati akiongea na waandishi wa habari katika viwanja vya mkuu wa Mkoa wa Kagera vilivyopo mjini Bukoba.
Msigwa alisema Kuhusu waliofariki, miili 16 imeshasafirishwa na kupelekwa maeneo ambayo wanafamilia walisema kwa kushirikiana na Kampuni ya ndege ya Precision kwa ajili ya maziko.
Alisema kati ya watu 19 waliofariki, watatu sio raia wa Tanzania mawasiliano yanaendelea ili miili hiyo pia iweze kusafirishwa kwenda kwenye nchi zao kwaajili ya mazishi.
Alisema marehemu wawili watapelekwa nchini Kenya na mmoja ni raia wa Uingereza.Alisema,ajali ni kitu ambacho hakina macho kinaweza kutokea wakati wowote.
“Niwahakikishie kwamba Serikali inaendelea kufanya juhudi kuhakikisha inaimarisha usalama katika usafiri wa anga katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, usafiri wa anga ni salama kuliko usafiri wowote”.alisema Msemaji huyo wa Serikali.
Alisema kitengo maalum cha uchunguzi wa ajali za anga kimeanza kazi yake tangu ajali ilipotokea, mpaka sasa kifaa cha mawasiliano kwa ajili ya kuwezesha uchunguzi kufanyika kimeshapatikana na taratibu za uchunguzi zinaendelea.
Aliongeza kuwa Wataalam kutoka Kampuni ya ATR ya nchini Ufaransa ambao ndio watengenezaji wa ndege iliyopata ajali wanatarajiwa kuwasili leo ili kuungana na timu ya wataalam waliopo, baadae timu ya watengenezaji wa injini watafika kwa ajili ya uchunguzi.
“Nawapongeza viongozi wa mkoa wa Kagera kwa kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha mara baada ya ajali hatua mbalimbali zilichukuliwa, nawapongeza sana wananchi wa mkoa huu hasa wavuvi kwa kazi kubwa ya kuokoa wenzetu”Aliongeza Msigwa.
Pia alisema taratibu za kumsajili kijana Jackson Majaliwa katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji zimeanza tayari ameshaandikishwa na atapelekwa wilayani Handeni mkoani Tanga kwa mafunzo ya miezi minne baada ya hapo anakuwa Askari wa Jeshi hilo.
Alisisitiza kuwa ,ajali haina kinga na inaweza kutokea mahali popote na mtu yeyote akiwa kwenye eneo ambalo ajali imetokea anao wajibu wa kusaidia kukabiliana na madhara ya ajali, ni moja kati ya misingi ya kukabiliana na majanga.
Alisema Serikali itaanza mara moja kununua vifaa na kuvipeleka maeneo mbalimbali ambapo majanga yanaweza kutokea.
“utafundisha wataalam na jamii juu ya namna bora ya kukabiliana na majanga”alisema.
Alisema Sasa hivi wameshajitokeza wachambuzi mbalimbali, kila mmoja anazungumza la kwake, natoa rai kwa Waandishi wa Habari tuwe weledi kwa kuchukua taarifa kwenye vyanzo sahihi kuhusiana na ajali hii ili kuepusha taharuki kwa wananchi.
Alisema Serikali haiwezi kuwa na dhamira ya kuacha Watanzania waangamie pale majanga yanapotokea, kwenye ajali hii tumejitahidi kuhakikisha tunatumia njia yoyote inayowezekana kuhakikisha kwamba tunapunguza madhara ya ajali.
“Nawapongeza Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amenituma niwaambie kwamba ameona kazi kubwa mnayoifanya ya kuhabarisha umma, anaomba muendelee kuwahabarisha na msiruhusu upotoshaji kufanyika”Alisisitiza.
“Kwa sasa tutabanwa na Sheria, kuna sheria ya kusimamia majanga ambayo itatuelekeza nini tunatakiwa tufanye na tunaendelea kuimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa ajili ya kukabiliana na majanga”aliongeza.
Alisema wanatarajia kuanza programu kubwa ya kutoa mafunzo kwa vijana na wadau juu ya namna ya kukabiliana na majanga na tunaendelea kuimarisha ofisi zetu za Zimamoto na Uokoaji ambapo katika bajeti ya mwaka 2022/23, zimetengwa Shilingi bilioni 9.9 kwa ajili ya kuboresha huduma katika eneo hilo.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi