November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ERB kujenga kituo kikubwa cha umahiri Dodoma kwajili ya ubunifu

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

BODI ya usajili wa Wahandisi Nchini (ERB) imesema kuwa Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 inatarajia kujenga kituo Kikubwa Cha Umahiri eneo la kizota, Jijini Dodoma ambapo ni Moja ya Vipaumbele vyake ili vijana waweze kufanya shughuli zao kwa kuonyesha ubunifu wao.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo na Msajili wa Bodi hiyo,Mhandisi Bernard Kavishe wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Majukumu ya Bodi ya usajili wa Wahandisi na Vipaumbele vyake kwa Mwaka wa fedha 2022/2023.

Ambapo amesema kituo hicho kitawafanya waendelee kukua lakini kitawasaidia Wahandisi kufanyakazi mbalimbali za kibunifu kwa umahiri zaidi.

Aidha Mha.Kavishe amebainisha kuwa Bodi hiyo ina Mpango wa Miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2025 yakiwemo mawili ya kitaifa.

Amesema lengo la kwanza ni kudhibiti maambukizi ya UKIMWI pamoja na magonjwa mengine ya kuambukiza.

“Hilo ni jukumu letu wote ili tuweze kujenga Taifa lazima tuwekeze kwenye afya,”amesema Mha.Kavishe.

Ametaja lengo la pili ni kupambana na Rushwa ambapo amesema bodi hiyo ipo mstari wa mbele katika kupambana na Rushwa maana yake rushwa ni adui wa uhai na kusisitiza kuwa sio tu adui wa haki bali ni adui wa uhai.

Amesema kuwa lengo mahususi la mpango huo ni kuimarisha udhibiti na utendaji kazi ya uhandisi na taaluma ya uhandisi kwasababu uhandisi hauishii shuleni bali mhandisi wanakwenda naye mpaka anapostaafu.

Mha.Kavishe ametaja lengo lingine ni kukuza na kuimarisha weledi ambapo amesema wanafanya Uimarishaji wa Taasisi yenyewe ili iweze kutoa huduma vizuri,lazima iwe imara.

Akizungumzia vipaumbele vya mwaka huu Mha.Kavishe amesema kuwa watahuisha leseni za wahandisi.

“Ili mhandisi aendelee kuwa shapu tunampa leseni na leseni ile kila baada ya miaka mitatu anabidi atuthibitishie kwamba anahuisha kwahiyo mwaka huu leseni zote zitakuwa zimefika mwisho wake na Wahandisi wanawajibika kuzihuisha,”amesema.

Hata hivyo amesema wanaendelea kuimarisha Taasisi  kwa upande wa sheria zinazoongozwa na taratibu na kanuni mbalimbali.

“Tunaendelea kudumisha nidhamu,kutoa elimu,kudhibiti hisibati katika vyuo vya elimu ya juu na vyuo vya ufundi sanifu,”amesema.

Vilevile,Mha.Kavishe amesema kuwa wanaendelea kupambana na vishoka wanaongilia mifumo na wanaoingilia taaluma.

“Tunaendelea kudhibiti wataalamu wanaotoka nje ya nchi lazima akija aje na ujuzi ambao sisi tunauhitaji lakini tunahakikisha kwamba utaalamu tunaoutaka uje umepita bodi kwahiyo kwajumla tunaimarisha,”amesema Mha.Kavishe.

Bodi ya Usajili wa Wahandisi ERB ilianzishwa Mwaka 1968 kwa mujibu wa Sheria namba15 kazi kubwa ni usajili Wahandisi na Kampuni na kudhibiti shughuli za kihandisi na lengo kubwa la Serikali ni kuangalia maslahi ya Umma hasa usalama kutokana na suala zima la udhibi wa Bodi hiyo ambapo hadi Sasa in ajumla ya wahandisi zaidi ya elfu30.