Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
CHUO cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP)kimeeleza utekelezaji na viapaumbe vya chuo hicho kwa mwaka 2022/23,ambapo kimesema hadi kufikia Juni 2022, jumla ya watumishi 351 walipata mafunzo ya muda mfupi na watumishi 50 wanaendelea na mafunzo ya muda mrefu ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo na Mkuu wa chuo hicho Prof.Hozen Mayaya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji na vipaumbele vyake ambapo amesema katika mwaka wa masomo 2021/22, chuo kimeendesha program za muda mrefu 31 na mpaka kufikia Juni 2022, washiriki 31 wa nje wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi.
“Kwa mwaka 2021/22, chuo kimesajili jumla ya wanafunzi 14,461 na jumla ya wahitimu 8,200 wamehitimu mwezi Disemba, 2021,”amesema.
Aidha Prof.Mayaya amesema katika mwaka wa fedha 2021/22, chuo kiliwezesha wahadhiri wake kufanya tafiti Saba zinazolenga kutatua matatizo ya kijamii, kiuchumi na kuchangia kuandaa sera na miongozo mbalimbali ya kitaifa.
“Chuo kinatekeleza mradi wa “Higher Education for Economic Transformation” ambao umetenga Shilingi bilioni 6.85 kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia, kujifunzia kwa kujenga jengo moja la taaluma, kuboresha mitaala na kuwajengea uwezo Wahadhiri,”amesema Prof.Mayaya.
Akizungumzia utekelezaji wa majukumu ya chuo hicho kwakipindi cha mwaka wa fedha 2021/22,Prof.Mayaya amesema kuwa chuo hicho kilitumia jumla ya Shilingi bilioni tisa zimetumika kugharamia utekelezaji wa miradi ya uendelezaji na utunzaji wa miundombinu ya chuo ambapo Shilingi bilioni tano zimetumika katika ujenzi wa kumbi Tatu za mihadhara na mabweni mawili ya wanafunzi wa kike.
Amefafanua kuwa Kati ya Shilingi bilioni tisa,Shilingi bilioni nne ambazo ni mapato ya ndani zimetumika kutekeleza miradi katika Kituo cha Mafunzo kilichopo Mwanza ikiwemo ujenzi wa mgahawa, jengo la utawala, maktaba na kununua ardhi kwa ajili ya upanuzi wa chuo.
Pia Prof.Mayaya amezungumzia vipaumbele vya chuo hicho kwa mwaka wa fedha 2022/23,amesema kuwa ni kuongeza udahili na usajili wa wanafunzi kutoka 14,417 mpaka kufikia wanafunzi 16,663 na kuendelea kufanya tafiti na kutoa huduma za ushauri na uelekezi kwa kufanya tafiti saba na kuandika kitabu kuhusu maendeleo vijijini.
Kipaumbele kingine ni Kuendelea kupitia mitaala ya mafunzo ya muda mrefu na kuandaa mitaala ya kozi mpya na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kujenga miundombinu ya kufundishia.
Pia Kuajiri watumishi wapya, kulipa stahili mbalimbali, kupandisha vyeo watumishi waliokidhi vigezo pamoja na kuboresha huduma za ustawi na kuongeza uwezo wa kielimu na kiutendaji kwa watumishi 396.
Pamoja na Kufanya ukarabati mkubwa na mdogo wa nyumba 13 za watumishi, kulipa madeni ya watumishi na watoa huduma, kutekeleza shughuli ambazo hazikutekelezwa katika Mpango Mkakati wa mwaka 2016/17-2020/21 pamoja na uendelezaji wa maeneo ya Miyuji Kaskazini, Chigongwe na Kiseke.
Pamoja na hayo ameeleza kuwa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kilianzishwa mwaka 1979 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuimarisha mfumo wa madaraka mikoani baada ya tafiti kuonesha watumishi wa ngazi mbalimbali kushindwa kutekeleza majukumu yao kutokana na kukosa mbinu na stadi za mipango ya maendeleo.
Huku madhumuni ya kuanzisha chuo hicho yakiwa ni kuboresha shughuli za upangaji mipango ya maendeleo vijijini kwa njia ya kuandaa wataalam wa mipango na kutoa mafunzo kwa watendaji na viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa.
More Stories
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe
Ilemela yakusanya bilioni 3.7.robo ya kwanza