November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia ameondoa mfumo dume, wanawake mjiamini- Waziri Mabula

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Dkt. Angeline Mabula amewataka wanawake kujiamini na kutumia fursa mbalimbali zinazowazunguka ili kujiimarisha kiuchumi badala ya kuendelea kulalamika kukwamishwa na mfumo dume.

Waziri Dkt. Mabula aliyasema hayo Oktoba 16, 2022 jijini Mwanza wakati akifungua kongamano la Jukwaa la Wanawake Viongozi wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kuongeza kuwa suala la mfumo dume nchini si changamoto kwani tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameliondoa.

“Hamtakiwi kuwa wanyonge tena, mjiamini kwani hakuna mfumo dume kwa sasa, wanawake tunaweza na hilo limedhihirishwa na Rais wetu Mhe. Rais Samia, ndiyo maana baada ya kuingia madarakani amepata tuzo mbalimbali kutokana na uchapaji kazi wake” alisisitiza Waziri Dkt. Mabula.

Aidha alisema Rais Samia ameendelea kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, akitolea mfano jijini Mwanza ambapo alisema soko kuu la Mwanza na Kirumba yatachochea fursa za kiuchumi kwa wananchi hususani wanawake ambao ni wengi masokoni.

Pia Dkt. Mabula aliwahimiza wanawake hao viongozi kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali ikiwemo za uzalishaji mali na kimafunzo na kisha kuwashirikisha wanawake wenzao kupitia vyama vya ushirika ili kusonga mbele kwa pamoja huku akiwahimiza kuwa tayari kuipokea sheria mpya ya bima ya afya kwa wote itakayorahisisha upatikanaji wa huduma bora za afya.

“Mkawe mabalozi wazuri wa kuelimisha wenzenu kuhusu bima ya afya kwa wote kwani kama huna uhakika wa afya yako, hutaweza kunufaika na fursa mbalimbali za uzalishaji mali. Kumbuka mlio hapa ni viongozi, mmeaminiwa na waliowachagua hivyo usifurahie tu kuwa kiongozi, bali kipindi chako kikiisha uwe umeacha alama” alidokeza Waziri Dkt. Mabula.

Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Antony Mavunde alitumia kongamano hilo kuwahimiza wanawake kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali akisema kwa sasa mpango uliopo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 nchi ijitosheleze kwa uzalishaji wa sukari na mafuta ya kula hivyo angetamani kuona wanawake wanachangamka kwa kuanzisha viwanda vidogo.

Naye Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Benson Ndiege alisema changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiwakumba wanawake ni mitaji ya uhakika kwa ajili ya kuanzisha miradi ya uzalishaji mali na hivyo kuwahimiza kutumia kongamano hilo kuweka mikakati ya pamoja ya kusonga mbele na kwamba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo iko tayari kuwasimamia.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Viongozi wa SACCOS, Monica Komba alisema awali wanawake waliathiriwa na kutojiamini kutokana na mfumo dume uliokuwa ukiwanyima fursa mbalimbali za kiuchumi lakini kupitia jukwaa hilo kumekuwa na mabadiliko makubwa ambapo kwa sasa wanashiriki shughuli mbalimbali na hivyo kuondokana na utegemezi.

Kongamano hilo limeambatana na kauli mbiu ya siku ya kimataifa ya ushirika inayoadhimishwa Oktoba 17, 2022 isemayo “Imarisha uwezo wako wa kifedha kwa siku zijazo kupitia ushirika wa akiba na mikopo”.
Na George Binagi, Mwanza
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Dkt. Angeline Mabula akizungumza kwenye kongamano la jukwaa la wanawake viongozi wa vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS) lililofanyika jijini Mwanza.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Dkt. Angeline Mabula akizungumza kwenye kongamano hilo. Waliokaa kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo Dkt. Antony Mavunde, Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika (SCCULT) Dkt. Cuthbert Msuya.
Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Antony Mavunde akitoa salamu zake kwenye kongamano hilo ambapo alisema bajeti ya Wizara hiyo imeongezeka kutoka Bilioni 294 kwa mwaka hadi kufikia Bilioni 954 mwaka 2022/23 na hivyo kutoa fursa kubwa ya kukuza sekta ya kilimo.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa Mwanza,  Emil Kasagala akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mawanza, Adam Malima wakati wa kongamano hilo ambapo aliwahimiza wanawake kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo jijini Mwanza ikiwemo za kiutalii.
Makamu Mwenyekiti Jukwaa la Wanawake Viongozi wa SACCOS, Monica Komba akizungumza kwenye kongamano hilo.
Makamu Mwenyekiti Jukwaa la Wanawake Viongozi wa SACCOS, Monica Komba. Waliokaa kutoka kulia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Dkt. Angeline Mabula, Naibu Waziri wa Kilimo Dkt. Antony Mavunde, Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika (SCCULT) Dkt. Cuthbert Msuya.
Wanawake viongozi wa SACCOS wakifuatilia kongamano hilo.
Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akitoa salamu kwenye kongamano hilo.
Picha ya pamoja.