April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Mbarawa: Viwanja vya Ndege vinaendelea kujengwa na kukarabatiwa

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Serikali inaendelea kuimarisha usafiri wa Anga ambapo Viwanja vya Ndege vyenye lengo la kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji vinaendelea kujengwa na kukarabatiwa katika Mikoa mbalimbali nchini.

Hayo ameyasema leo (Agosti,4, 2022) Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa wakati akitoa ufafanuzi wa Bajeti ya wizara ya ujenzi na uchukuzi na utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23 na kusema kuwa hadi sasa, Serikali ina jumla ya Viwanja vya Ndege 58 vilivyo chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na kimoja (1) kilicho chini ya KADCO.

“Serikali imepanga kuendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Mtwara, Songwe, Geita, Iringa, Msalato, Musoma na Songea. Aidha, Serikali inatarajiwa kuanza utekelezaji wa miradi mipya ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Ndege vya Kigoma, Tabora, Sumbawanga na Shinyanga. Vilevile, Serikali inaendelea na maandalizi ya miradi ya ujenzi, ukarabati na upanuzi wa viwanja vya Ndege vya Njombe, Lindi, Mpanda, Lake Manyara, Bukoba, Moshi, Tanga, Simiyu, Mwanza (Jengo jipya la abiria), Arusha pamoja na viwanja vingine vya Ndege vya mikoa.”

Pia Prof. Mbarawa amesema hadi kufikia Mei, 2022, Serikali ilikamilisha ununuzi wa ndege tatu (3) mpya na kuzikabidhi ATCL na kuendelea kutumika. Ndege hizo ni Dash 8 Q400 ndege moja (01) yenye uwezo wa kubeba abiria 76 na ndege mbili (2) aina ya Airbus A220-300 zenye uwezo wa kubeba abiria 132 kila moja. Kuongezeka kwa ndege hizo kumeifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege mpya 11 ikilinganishwa na ndege 8 zilizokuwepo mwaka 2020/2021.

Kuhusu Bajeti ya Sekta ya Uchukuzi katika mwaka wa fedha 2022/23 pamoja na mambo mengine inalenga kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ambayo itakuwa na matokeo chanya makubwa katika Sekta nyingine za kiuchumi na kijamii.

“Miradi hiyo ni pamoja na: Ujenzi wa Reli ya Standard Gauge (SGR); Ujenzi na ukarabati wa Barabara, Uboreshaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania; na Ujenzi na Ukarabati wa Meli katika Maziwa Makuu. Aidha, maeneo mengine yaliyopewa kipaumbele katika mwaka wa fedha 2022/2023 ni pamoja na Ukarabati wa miundombinu ya reli iliyopo; Uboreshaji wa bandari; Uboreshaji wa huduma za usafiri wa anga, maji na nchi kavu; Uboreshaji wa huduma za hali ya hewa; na uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia katika vyuo vya mafunzo ya Sekta za Ujenzi na Uchukuzi. “

Aidha Prof. Mbarawa amesema Serikali inaendelea kutoa huduma ya Vivuko vinavyotumia Engine ambavyo vinafikia 33 katika maeneo 22 hapa nchini na Boti 7 zinazotoa huduma katika maeneo mbalimbali wakati wa dharura ambapo mwaka huu Serikali imepanga kununua vivuko vipya Saba (7) ambavyo Magogoni – Kigamboni, Kisorya- Rugezi, Ijinga-Kahangala, Biro- Bukondo, Nyakarilo- Kome, Buyangu- Mbalika na Nyamisati – Mafia.

Pia Prof. Mbarawa amesema Katika kipindi hiki, Serikali bado inaendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara zenye urefu wa kilometa 1,593 ambazo zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Baadhi ya miradi inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za Mzunguko wa Nje katika jiji la Dodoma (Dodoma Outer Ring Road km 112.3); Uvinza – Malagarasi (km 51); Kabingo – Kibondo Town – Kasulu – Manyovu (km 286.5); Pangani – Tanga (km 50); Mkange – Tungamaa – Pangani (km 120.8), Daraja la Pangani (m 525).

Mbali na hayo Prof. Mbarawa amesema Serikali bado inaendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara zenye urefu wa kilometa 1,593 ambazo zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

“Baadhi ya miradi inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za Mzunguko wa Nje katika jiji la Dodoma (Dodoma Outer Ring Road km 112.3); Uvinza – Malagarasi (km 51); Kabingo – Kibondo Town – Kasulu – Manyovu (km 286.5); Pangani – Tanga (km 50); Mkange – Tungamaa – Pangani (km 120.8), Daraja la Pangani (m 525).”

Prof. Mbarawa amesema Sera ya Serikali ni kuunganisha Makao Makuu ya mikoa yote nchini, ambapo hadi sasa mikoa yote imeungwa kwa barabara za lami isipokuwa mikoa michache ambayo hata hivyo Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya barabara za kuunganisha mikoa hiyo.

Mbali na hayo Prof. Mbarawa amesema utekelezaji wa miradi ya kupunguza msongamano katika jiji la Dar es salaam ikiwemo barabara za Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Pili (Mbagala hadi katikati ya Jiji la Dar es Salaam – km 20.3) na Awamu ya Tatu (Gongo la Mboto hadi katikati ya Jiji la Dar es Salaam – km 23.33) unaendelea ambapo Mkandarasi yupo katika maandalizi ya kuanza kazi za ujenzi (mobilisation).

“Miradi mingine itakayotekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia ni pamoja na Lusahunga – Rusumo (km 92), Mtwanga – Mingoyo – Masasi (km 201), Iringa – Msembe (km 104), Rutikila – Songea (km 95) na Songea Bypass (km 15)”