November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TBS kujenga Maabara ya Bilioni 9.9 Dodoma kuhudumia Miji ya Kimkakati

TBS kujenga Maabara ya Bilioni 9.9 Dodoma kuhudumia Miji ya Kimkakati.

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la viwango Tanzania (TBS) Dkt.Athuman Ngenya amesema ili kusogeza huduma karibu na wananchi shirika hilo limeanza ujenzi wa jengo la Maabara Jijini hapa lenye thamani ya shilingi Bilioni 9.9 ili kuhudumia Miji ya Kimkakati(Viwango House).

Dkt.Ngenya amesema hayo jijini hapa leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Mwaka wa fedha wa 2022/2023 ambapo amesema kuwa kwa sasa Maabara ipo Moja tu ya Dar-es-salaam makao mkuu jambo ambalo linasababisha kucheleweshwa kwa huduma hivyo wanajenga maabara hiyo ili kuhudumia wafanyabiashara na wajasiriamali wa Mikoa ya Mwanza na Dodoma.

Dkt.Ngenya amesema kuwa katika kuhakikisha usalama wa vyakula na vipodozi kwa Taifa unakuwpo shirika limeona ni vyema kujenga maabara hiyo ambayo hadi sasa imefikia asilimia 20 na kutarajiwa kukamilika miaka miwili ijayo.

“Ili kuondasha ile adha iliyopo kwa sasa ya kusafiri kutoka mbali kupeleka bidhaa maabara kuu ya Dar-es-salaam kupima ubora na itasaidia pia kuharakisha maendeleo ya watoa huduma,

“Unakuta mtu anatengeneza mkate wake huko Kagera sasa ili kupitishwa kwa ajili ya kuingizwa sokoni kwa maana ya kuanza kutumika na wananchi ni lazima asafirishe mpaka Dar-es-salaam kwa ajili ya kupimwa ubora sasa embu fikiria kutoka Kagera mpaka Dar-es-salaam hapa katikati inaweza ikatokea chochote ikaoza ama ikapata changamoto sasa unakuwa umepoteza muda,”amesema Dkt.Ngenya

Pia Dkt.Ngenya amesema Shirika limetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya kuimarisha ofisi saba za kanda za shirika katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma na Mbeya.

Fedha hizo pia zitatumika kuimarisha ofisi za shirika hilo mipakani ikiwemo Tunduma, Kasumulo, Horohoro, Holili, Tarakea, Namanga, Bandari ya Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro,Sirari, Kabanga, Rusumo, Mtukula, Bandari ya bagamoyo, bandari ya Dar es salaam, uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere- Dar, Bandari ya Tanga)

“Pia tutaongeza wafanyakazi na vitendea kazi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakati na kuimarisha zoezi la ukaguzi wa mara kwa mara sokoni ili kupunguza bidhaa hafifu sokoni na hatimaye kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa bora na salama” amesema Dkt.Ngenya

Amesema pia shirika hilo limetenga shilingi bilioni 1.6  kwa ajili ya kuandaa viwango 630 vya kitaifa katika sekta mbalimbali ili kuwezesha biashara kwa kumpa uhakika mzalishaji wa kupata masoko ya ndani na nje, kumhakikishia mlaji wa mwisho usalama na ubora wa bidhaa atakayotumia ikiwa ni pamoja na kuweka ushindani sawia wa bidhaa katika soko.

Dkt.Ngenya ameeleza kuwa ili kuhakikisha wananchi wanatumia bidhaa zilizo bora na salama Shirika hilo pia limetenga milioni 261 kwa ajili ya kuimarisha shughuli za usajili wa bidhaa na majengo ya chakula na vipodozi.

Dkt.Ngenya ameeleza kuwa Shirika hilo pia limetenga shilingi 581 Millioni kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uthibitishaji wa mifumo ya kiutendaji ambapo kwa sasa TBS imepatiwa ithibati ya kufanya shughuli hiyo na mashirika yanaweza kuthibitishiwa ubora wa mifumo yao ya kiutendaji kupitia hii itasaidia kuhakikisha wananchi wanapokea huduma zilizo bora.

Amesema Katika kufanya shughuli za kuhakiki ubora wa vipimo ili kuhakikisha usahihi wa majibu ya vipimo mbalimbali kutokea maabara, mahospitalini na viwandani na kupelekea watoa huduma au maamuzi kufanya maamuzi sahihi Shirika hilo limetenga TZS 800 Millioni.

Shirika limetenga TZS 1.18 Billioni kwa ajili ya kuimarisha shughuli za ukaguzi wa bidhaa kabla ya kusafirishwa kuja nchini (PVoC) na baada ya kuwasili nchini (Destination Inspection) ili kuhakikisha nchi haiwi jalala la kupokea bidhaa zilizopigwa marufuku au hafifu.

Shirika la viwango Tanznania (TBS) linaendelea na juhudi za kuweka na kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuboresha huduma zake kwa lengo la kuwezesha biashara kwa dhumuni la kuinua uchumi wa viwanda kwa kuchagiza uzalishaji wa bidhaa salama na bora hapa nchini kama njia mojawapo ya kuchangia pato la Taifa letu.