November 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania kunufaika na wenyeji wa mkutano wa 65 wa UNWTO

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Tanzania inatarajia kunufaika na fursa mbalimbali zitakazotokana na Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani UNWTO – CAF utakaofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 7, 2022.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alipokua akizungumza na vyombo vya habari jijini Arusha kuhusu kufanyika kwa mkutano huo ambapo amesema Tanzania itanufaika na ujio wa mkutano huo kwa kukuza na kuendeleza utalii, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa pamoja na lengo litakalowekwa la haki ya msingi ya binadamu kutembelea maeneo mbalimbali ya
vivutio vya Utalii bila vikwazo vyovyote.

Kuhusu mkutano huo Mhe. Waziri Balozi Pindi Chana amesema utahudhuriwa na watu mashuhuri wakiwemo Katibu Mkuu wa UNWTO, Mawaziri wa Utalii kutoka nchi Wanachama wa Shirika la Utalii Duniani – Kamisheni ya Afrika na wadau wa utalii kutoka ndani na nje ya Afrika na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.

“Mkutano huu utahusisha matukio mbalimbali ikiwemo Mkutano wa Mawaziri wa Utalii kutoka nchi wanachama, Jukwaa la Uwekezaji kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini na mafunzo kwa wadau wa sekta ya Utalii yaani Marketing Symposium kwa lengo la kuwajengea uwezo wadau wa utalii kuhusu utangazaji Utalii”. Amefafanua Waziri Chana

Aidha, kwa kutambua umuhimu wa mkutano huo, Mhe Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa rai kwa wadau wote wa utalii hususan wakazi wa Jiji la Arusha na maeneo ya jirani wanaotoa huduma za malazi, mawakala wa biashara za utalii, na waongoza watalii kuonesha ukarimu wa hali ya juu kwa washiriki wa Mkutano wa 65 wa UNWTO – CAF kwa kipindi chote watakachokuwa hapa nchini ili waitangaze vyema
Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya UNWTO, Mkurugenzi wa Shirika la Utalii Duniani Kamisheni ya Afrika Bi. Marie Elicie, amesema wameridhishwa na namna Tanzania ilivyo jiandaa kwa mkutano huo wa Kimataifa kuanzia viwanja vya ndege, hoteli na ukarimu kwa watoa huduma.

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Pindi akizungumza na Waandishi wa habari
,jijini Arusha.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Pindi akizungumza Mkurugenzi wa Shirika
la Utalii Duniani Kamisheni ya Afrika Bi. Marie Elicie mara baada ya kumaliza
kuongea na Waandishi wa Habari.
Picha ya pamoja na Wajumbe wa kamati ya Taifa ya maandalizi ya Mkutano
wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani UNWTO – CAF