Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Lushoto
MKUU wa Shule ya Sekondari ya Wasichana St. Mary’s Mazinde Juu iliyopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Mtawa Evetha Kilamba, amesema siri ya mafanikio ya shule hiyo, ambapo wanafunzi saba wameingia kwenye 10 bora kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2022, ni nidhamu iliyojengwa kwa pamoja kati ya wanafunzi, walimu na wazazi.
Lakini pia, uwajibikaji wa pamoja kati ya wanafunzi, walimu na wazazi, umechangia mafanikio hayo, kwani kauli mbiu ya shule hiyo ‘Kwa Moyo Wote’ kunampa nafasi kila mmoja kufanya kile anachoweza kwa uwezo wake wote kuona anafanikisha malengo yake, na ya wengine.
Aliyasema hayo Julai 6, 2022 wakati anazungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake baada ya Julai 5, 2022, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) Athuman Amas kutangaza matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka 2022.
“Nidhamu ya wanafunzi, wazazi na walimu ndiyo imechangia mafanikio haya ambayo yametufikisha hapa. Wanafunzi wamekuwa wanatumia muda wao vizuri kuona wanasoma kwa bidii, na hawafanyi mchezo mchezo wakiwa shuleni. Lakini pia wazazi wamekuwa wanatuunga mkono kwa kulipa ada na mambo mengine.
“Na sisi (Jumuiya ya Shule) kama taasisi ya kidini, tuna hofu ya Mungu. Hatuwezi kuchukua ada halafu walimu wetu wasifundishe. Ni lazima tuwasimamie na kuona matarajio ya wazazi ambao wameamua kuwalipia ada watoto wao, basi wanafaulu vizuri” alisema Kilamba.
Kilamba alisema, pia mafanikio yamechangiwa na ufuatiliaji wa wanafunzi hao kwa kila siku, na kuona kila mmoja anafanya vizuri kwenye masomo yake. Na hiyo ni kwa sababu shule yao haifanyi mchujo kwa wanafunzi waliofanya vizuri ama vibaya, hivyo wanachokifanya hapo ni kuhakikisha wote wanafanya vizuri.
“Tunafuatilia sana maendeleo ya mwanafunzi, na kama yupo chini kiuwezo katika masomo, anasaidiwa mpaka anafaulu. Sisi St. Mary’s Mazinde Juu tunajali wanafunzi wote, na kuona wanafanya vizuri.
“Na katika malezi ya watoto hapa shuleni, kila siku tunaanza na sala asubuhi. Na hawasomi tu, bali tunawafundisha kujitegemea, wanafanya kazi za mikono ikiwemo kushona, kutunza mifugo ikiwemo ng’ombe, kuku na nguruwe. Pia wanafanya usafi kwenye madarasa yao, na kufanya usafi wao wenyewe, bila kusahau kufanya mazoezi asubuhi na kushiriki michezo” alisema Mtawa Kilamba.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mwanafunzi bora kitaifa wa kidato cha sita mwaka 2022, Catherine Mwakasege ambaye pia anatoka Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St. Mary’s Mazinde Juu, alisema malengo yake ya kusomea udaktari Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili (MUHAS) yametimia, na anamshukuru Mungu, kwani matarajio yake ilikuwa kufaulu tu, lakini Mungu amemfanya kuwa wa kwanza kitaifa.
Mama mzazi wa Catherine, Lida Mahundi alisema anamshukuru Mungu kwa mtoto wake kufanya vizuri, kwani huyo ni mtoto wake wa pili kufanya vizuri kitaifa, lakini huyo amepitiliza, kwani ameongoza nchi nzima kwa kufanya vizuri matokeo ya kidato cha sita mwaka huu.
Baba mzazi wa Catherine, Alphonce Mwakasege alisema shukrani za kwanza ziende kwa Mwenye Enzi Mungu, za pili ziende kwa walimu wa mwanafunzi, za tatu kwa mwanafunzi, na mwisho ndiyo ziende kwa wao wazazi, kwani mafanikio ya mtoto wao yamepitia kwenye mikono mingi.
More Stories
Rais Samia amlilia Dkt. Ndugulile
Makada wa CHADEMA,mbaroni kwa tuhuma za kukimbia na karatasi za kuraÂ
Rais Samia afanya uteuzi wa viongozi mbalimbali