November 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wabunge Vinara wa mapambano ya TB kuendelea kutoa elimu dhidi ya ugonjwa huo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mtandao wa Wabunge Vinara wa Mapambano dhidi ya Kifua Kikuu wametakiwa kuendelea kutoa elimu kuhusu ugonjwa huo wanaporudi majimboni

Hayo yamesemwa na Naibu Mwenyekiti Mhe. Sebastian Kapufi wakati wa semina kwa wabunge hao iliyoandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP)

Mhe. Kafupi alisema kuwa suala la uelewa kuhusu Kifua Kifua bado ni mdogo katika jamii hivyo kupelekea kushamiri kwa unyanyapaa kwa wagoniwa wa Kifua Kikuu.

“Majukumu ya wajumbe wa mtandao huo yamebainishwa ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi kwani bado kuna uelewa mdogo kwa jamii na hivyo kupelekea unyanyapaa”.Alisema Mhe.Kafupi

Aliongeza kusema kuwa bado kuna uhitaji wa mikakati ya makusudi ya kudhibiti Kifua Kikuu hasa katika maeneo ya migodi ambako wachimbaji wadogo wadogo wanapatikana.

Alisema kwa kutoa elimu ya kupambana na ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa wachimbaji hao ambao wengi wao ni waathirika wa ugonjwa huo itasaidia jamii nzima inayowazunguka kuelewa Kifua Kikuu kinatibika .

kwa upande wa Meneja Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma, Dkt. Riziki Kisonga alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuendelea kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2025 kutoka ile ya awali ya asilimia 52 ya mwaka 2020.

Aidha, Dkt.Kisonga aliwashukuru na kuwapongeza Wabunge hao kwa kujitoa kwao katika mapambano dhidi ya TB na kuwaomba waendelee kushirikiana na Wizara katika kuondoa unyanyapaa uliopo kwenye jamii dhidi ya wagonjwa wa Kifua Kikuu.