Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga
IDARA ya Uhamiaji mkoani Shinyanga imewaonya wakazi wa mkoa huo kujiepusha na tabia ya kuwapokea na kuwahifadhi wahamiaji nchini kwa lengo la kujipatia fedha kitendo ambacho kinaweza kusababisha wachukulie hatua kali za kisheria.
Onyo hilo limetolewa na Ofisa Uhamiaji mkoa wa Shinyanga, Rashidi Magetta alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na kuongezeka kwa matukio ya kukamatwa kwa wahamiaji haramu katika maeneo mbalimbali nchini.
Magetta anasema mtu ye yote anayepokea na kuwahifadhi raia wa kigeni wanaoingia nchini kinyume cha sheria anakuwa ametenda kosa na iwapo atafikishwa mahakamani na kutiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyopungua shilingi milioni 20 au kifungo cha miaka 20 gerezani.
Anasema katika kuhakikisha wananchi wanaepukana na vitendo hivyo Idara ya uhamiaji mkoani Shinyanga imeanzisha kampeni maalumu ya kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na suala zima la kujiepusha na vitendo vya kupokea na kuwahifadhi wahamiaji haramu tendo ambalo ni la uvunjaji wa sheria za nchi.
Magetta anaendelea kueleza kuwa dhima ya kampeni hiyo ni katika kutekeleza “Ulinzi Shirikishi” katika suala zima la kuwabaini wahamiaji haramu wanaoingia nchini kinyemela ambao mara nyingi hupata msaada wa wenyeji (mawakala) wanaowapokea na kuwapitisha kwenye njia za panya kukwepa mikono ya Serikali.
Akifafanua Magetta anasema wengi wa wahamiaji haramu wanaoingia nchini kinyume cha sheria mara nyingi hawaaminiki na wengi wao hujiingiza kwenye vitendo vya kiuhalifu ambavyo husababisha madhara kwa raia wasiokuwa na hatia.
“Yapo madhara ya wahamiaji haramu ya muda mfupi na muda mrefu lakini wananchi wanapaswa kuelewa, wengi wa wahamiaji haramu huingia nchini kwa maslahi yao binafsi na mara nyingi wanaweza kujiingiza kwenye vitendo vya ujasusi dhidi ya nchi yetu,”
“Kwa kifupi suala la wahamiaji haramu ni mtambuka, linavuta hisia za wananchi kwa ujumla lakini tukumbuke kuwa dunia yote inashuhudia matumizi makubwa ya kudhibiti wahamiaji haramu wanaosafarishwa kutoka sehemu moja ya dunia hadi nyingine,” anaeleza Magetta.
Anasema tatizo la wimbi la uingiaji wahamiaji haramu hapa nchini bado ni kubwa na linahitaji nguvu kubwa tena ya pamoja, na mikakati mbalimbali katika kuhakikisha wahamiaji wanaoingia nchini kwa njia za panya wanadhibitiwa.
Magetta anasema kampeni inayoendelea hivi sasa ni kuwahimiza wananchi kuwatambua majirani zao wote ili inapotokea kumuona mtu wasiyemfahamu au kumtilia shaka waweze kutoa taarifa katika vyombo vya dola aweze kukamatwa na kuhojiwa uraia wake.
“Tunaposema kila mtu amtambue jirani yake ni kati ya njia nyingi ambazo Idara yetu ya Uhamiaji nchini inajaribu kuja nazo katika suala zima la kupambana na wahamiaji haramu, maana wengi wao wanapoingia nchini hupokelewa na wenyeji na kuhifadhiwa kwa siri,”
“Ni muhimu wananchi wawe makini na waangalifu kwa raia wote wanaotoka nje ya nchi yetu, hasa wageni wanaoingia kwa vibali maalum vya kufanya kazi za muda, inabidi wafuatiliwe iwapo vibali walivyonavyo havijamaliza muda wake, maana baadhi huingia kwa kigezo cha kazi na baadae hubaki nchini moja kwa moja,” anaeleza.
Anasema muarobaini wa tatizo la wahamiaji haramu hapa nchini ni kutekeleza dhana ya Mwananchi Mtambue Jirani yako, Toa taarifa na zingatia utekelezaji wake na ni muhimu wananchi wakawa makini na waangalifu kwa raia kutoka nje ya nchi wachukuliwe kwa umuhimu wa shughuli wanazokuja kufanya kwa muda mahususi.
Mwisho.Maelezo ya Picha1. Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Shinyanga, Rashidi Magetta.2. Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji Mkoani Shinyanga (Picha na Suleiman Abeid).3. Wahamiaji haramu ambao wamewahi kukamatwa hapa nchini kinyume cha sheria (Picha kwa hisani ya mitandao ya kijamii)
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi