Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Uanzishwaji wa kituo cha pamoja(one stop center) ni jitihada za serikali katika kuhakikisha waathirika wa vitendo vya ukatili hususani wa watoto wanapata huduma muhimu ikiwemo matibabu.
Kupatikana kwa huduma zote kwa pamoja imesaidia sana watoto ambao ni waathirika wa vitendo vya ukatili kuweza kukingwa na maambukizi ya maradhi mbalimbali kama Ukimwi,magonjwa ya zinaa pamoja na mimba.
Akizungumza na timesmajira online ofisini kwake Ofisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure, Hellen Gabriel ameeleza kuwa kupitia kituo chao cha one stop center katika hospitali hiyo wamesaidia watoto wengi ambao ni waathirika wa vitendo vya ukatili hususani kubakwa ili wasiweze kupata maambukizi ya magonjwa.
“Kupitia one stop center watoto wengi tumenawaokoa akiwai ndani ya masaa 72 kwa kumkinga asipate maambukizi ya magonjwa ya zinaa,Ukimwi,mimba katika umri mdogo kwa sababu kuna dawa ambazo zinazuia vitu kama hivyo ambazo utolewa na wataalamu wa afya kwa ajili ya kumkinga muathirika wa vitendo vya ukatili asipate maambukizi,ni kitu kizuri kuanzishwa kote ili waathirika wa vitendo vya ukatili hususani watoto waweze kufika kwa uharaka na kupatiwa huduma zote kwa pamoja kwani kabla ya kuanzishwa kwa vituo hivyo watoto walijikuta wanapata maambukizi na mimba kwani wakizunguka muda mrefu kufuata huduma,”ameeleza Hellen.
Hellen ameeleza kuwa wanaenda kwenye jamii ikiwemo shuleni kuwafundisha watoto kuwa ukatili ni nini na one stop center ni nini na wakifanyiwa ukatili wakimbilie katika vituo hivyo ili waweze kupata huduma na kuwaokoa ndani ya masaa 72 na magonjwa.
Ofisa Ustawi wa Jamii kituo cha pamoja(One stop center) kilichopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure Godlove Lulandala, ameeleza,kituo hicho kimeanzishwa kwa lengo la kurahisisha huduma za kimatibabu kwa waathirika wa vitendo kwa ukatili ikiwemo watoto ambao ndio wamekuwa wahanga zaidi.
“Huduma zote za kipolisi,kimatibabu na kiustawi zinapatikana katika eneo moja ambapo zamani zilikuwa zinasababisha mtu azunguke kwa muda mrefu sana,inarahisisha hupatikanaji wa taarifa muhimu ambazo zitahitajika wakati muathirika amefanyiwa tukio zamani wakati mtu anazunguka kuna baadhi ya taarifa zilikuwa zinapotea ikiwemo zile zinazohitajika kwa ajili ya kisheria na kufungua kesi,”ameeleza Lulandala.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Ramadhan Ng’anzi,akizungumza na timesmajira ofisini kwake mkoani hapa, ameelezea namna one stop center imekuwa suluhisho kwa waathirika wa vitendo vya ukatili kupata matibabu na huduma za kipolisi kwa wakati mmoja.
Ng’anzi, ameeleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa kituo cha pamoja kulikuwa na tatizo kwa waathirika wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji kupata huduma ya matibabu kwa haraka kwani ilimlazimu aanzie Polisi.
Daktari akimpata mtu aliyepata madhara kutokana na unyanyasaji wa aina yoyote ile inabidi kabla ya kumpatia matibabu lazima amtake muathirika wa vitendo hivyo kuleta Fomu namba tatu ya Polisi(PF3),kwa sababu baadhi ya hospitali na vituo vya Polisi vina umbali mrefu ikaonekana kwamba huyu muathirika anapata shida.
“Jeshi la Polisi na Wizara ya Afya pamoja na Ustawi wa Jamii wakaamua watengeneze kitu ambacho kitamrahisishia huyu mwananchi kupata huduma kwa urahisi ndio likaja wazo la kuanzisha kituo cha pamoja(one stop center), ambapo Polisi na watoa matibabu wapo eneo moja hivyo muathirika wa vitendo hivyo anapata huduma za kipolisi na matibabu katika eneo moja,”ameeleza Ng’anzi.
Ameeleza kuwa Jeshi la Polisi kwa kufanya tathimini mbalimbali wanaona wamefanikiwa kwa sababu kwanza mtu akipata madhara yoyote anawai hospitalini ambapo hapati urasimu wa aina yoyote anapata huduma kwa haraka na kuokoa maisha yake.
Mbali na hayo pia ameeleza kuwa one stop center imekuwa msaada kitakwimu ambapo wanaweza kukusanya takwimu za vitendo mbalimbali vya ukatili na kuzipeleka katika Jeshi la Polisi ili waweze kuangalia vitendo hivyo vinapanda au vinashuka na kuweza kufungua kesi.
“Licha ya kwamba muathirika wa vitendo hivyo anapata huduma haraka lakini sisi pia na wenzetu wa afya kitakwimu inatusaidia kukusanya taarifa za namna hiyo, kuja kituo cha Polisi kufungua kesi kwamba labda huyu amepigwa,huyu amebakwa na huyu amefanyiwa hivi,na Polisi wetu yupo kama jicho letu la kipolisi katika kituo hicho atatupa taarifa na sisi tutachukua hatua za haraka sana za kufungua kesi,”ameeleza Ng’anzi.
Aidha ameeleza kuwa mwitikio wa jamii ni mzuri katika kwenda kupata huduma kwenye vituo vya pamoja baada ya kuona hakuna urasimu tena.
“Katika Mkoa wa Mwanza kila Wilaya na vituo vya afya tumeweka vituo vya namna hiyo na kwa hapa jijini Mwanza one stop center ipo katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure,kwaio wananchi wa Mkoa wafike katika hospitali za Wilaya na kama ziko mbali basi waende kwenye vituo vya afya vile vile wanaweza kupata huduma ya one stop center,”.
Naye Ofisa Mradi wa shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence Elihaika Mugenyi,ameeleza kuwa wameona serikali iliweka jitihada za kuanzisha one stop center ambayo imekuwa msaada kwa waathirika wa vitendo vya ukatili kupata haki zao ikiwemo matibabu kwa uharaka.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili