Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa(Takukuru) Mkoa wa Mbeya inaendelea kumshikilia Mtalaam wa mionzi katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mbeya , Labert Haule kwa kudaiwa kujifanya ofisa Takukuru na kuchukua fedha kwa wananchi kwa madai ya kuwasaidia kesi zao ili waachiwe huru na kufutiwa mashtaka yanayowakabili.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Takukuru mkoa wa Mbeya ,Maghela Ndimbo amesema hayo leo wakati akitoa taarifa ya miezi mitatu kutoka mwezi Januari hadi marchi mwaka huu.
Ndimbo amesema kuwa tayari wamemkata mtalaam huyo ila wanasubiri kibali toka kwa mkurugenzi wa mashtaka mara baada ya uchunguzi kukamilika na kupata kibali ili aweze kufikishwa mahakamani .
“Hivi sasa sheria imebadilika sana mtu yeyote akikamatwa lazima uchunguzi ukamilike kwanza tofauti na zamani mtu anakamatwa anapelekwa mahakamani huku uchunguzi ukiendelea kufanyika hivi sasa haipo hivyo”amesema Mkuu huyo wa Takukuru .
Hata hivyo Mkuu huyo Takukuru amesema kwamba mara nyingi watu wanaojifanya maafisa Takukuru wamekuwa wakitumia simu ambazo wamesajili kwa majina yasiyo yao kufanya matukio hayo ya udanganyifu kwa wananchi na pale wananchi wanapohitaji kuonana nao huwa hawakubali na kudai fedha watumiwe kwa njia ya simu ambazo wamesajili kwa majina ambao siyo yao .
Aidha Ndimbo ametoa onyo kwa watu wanaojifanya maafisa Takukuru kwa kuwalaghai wananchi kuwa wana uwezo wa kuwasaidia kutokana na na kutuhumiwa kwa makosa mbali mbali ili waachiwe na kufuta mashtaka ya uongo wanayodai yanayowakabili baadhi ya wananchi .
Akielezea zaidi Ndimbo amesema kuwa watu hao wanaojifanya maafisa wa Takukuru wamekuwa wakiwasingizia wananchi kadhaa kuwa wanakabiliwa na mashtaka ya Rushwa TAKUKURU wakati sio kweli na hatimaye kuwaomba fedha ili wawasaidie haja yao ni kuwatapeli kwani hawawezi kulifanya.
“Takukuru ipo kazini inaendelea na uchunguzi wa kuwatafuta watu hao watakamatwa na hatimaye kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria , tumebaini kuwa vitendo hivi vimekuwa vingi lazima watu hawa tuwakamate”amesema Ndimbo.
Aidha Mkuu huyo wa Takukuru amesema kuwa katika kipindi cha miezi mitatu waliweza kufanya uchunguzi sekta ya elimu kwa upande wa walimu kujihusisha na rushwa ya ngono na wasimamizi wa sekta ambapo walibaini mapungufu kadhaa ikiwemo ukosefu wa maadili kwa baadhi ya watumishi wa sekta ya delimu kujirahisi kwa walimu wa kike ili waweze kupangiwa shule zilizoko mjini na kutaka madaraka bila kufuata utaratibu.
Ndimbo amesema kuwa baada ya kubaini mapungufu hayo walikaa vikao na wadau wa sekta ya elimu kwa ajili ya kuondoa mianya ya rushwa iliyobainika na kuwekeana mikakati ya ufuatiliaji .
Amesema kuwa tayari wamefanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo (26) yenye thamani ya Bil.18 ambapo miradi hiyo ni Afya, Elimu,Maji,Barabara na madini ambayo ilikuwa na changamoto ya utekelezaji.
“Kati ya miradi hiyo baadhi tulikuta ina kasaro kubwa zilizosababisha uchunguzi kuanzishwa ni mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Mbarali ambapo awamu ya kwanza ulikuwa na thamani ya zaidi ya Bl.2.500”amesema .
Alisema baada ya ufuatiliji wa kina mradi huo ulikutwa na kasoro kadhaa ikiwemo kujengwa chini ya kiwango na hivyo kuifanya Takukuru mkoa wa Mbeya kuanzisha uchunguzi wamatumizi halisi ya fedha zilizotumika kutekeleza mradi huo.
Amesema kuwa mradi mwingine uliofutiliwa ni ujenzi wa Mzani wa barabara ya Makongorosi Chunya wenye thamani ya shilingi 7,539 Bilioni na kulazimika kuanzisha uchunguzi baada ya kubaini kutengwa kiasi kikubwa cha fedha kuliko uhalisia.
“ Tumebaini kuwepo kwa changamoto ya malalamiko kutoka kwa wananchi ya uwepo wa malipo hewa ya fidia kwa waliopisha maeneo yao ili kupisha mradi huo uweze kujengwa hivyo Takukuru tayari imeanzisha uchunguzi wa tuhuma hizo.
Akizungumzia kuhusu watu wanaojifanya maafisa Takukuru ,Mkazi wa Sai Jijini Mbeya Faraja Juma amesema kuwa suala la maafisa vishoka limekuwa kero katika maeneo mbali mbali hasa kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya pembezoni .
“Tunashukuru Takukuru wameliona hili tunaomba watusaidie tunaliwa sana hela na hawa watu na wanachukua fedha nyingi kwa madai ya kutusaidia “amesema faraja.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba