November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mliokaa madarakani muda mrefu jitafakarini kabla ya kuondolewa kwa aibu asema RC

Na Israel Mwaisaka,TimesMajira Online

Mkuu wa mkoa Rukwa Joachimu Wangabo amewataka madiwani waliokaa muda mrefu katika nafasi hiyo kufikiria zaidi kustaafu nafasi hizo badala ya kusubiri kuondolewa kwa aibu kwenye mchakato wa uchaguzi na kuwa hiyo itawajengea heshima kubwa.

Kauli hiyo ameitoa leo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya Nkasi kilicholenga kujadili hoja za ukaguzi ambapo amedai kuwa, kimesalia kikao kimoja cha baraza hilo kuvunjwa kwa ajili ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu na kuwa sasa ni wakati wa kila mmoja kujitafakari nini amefanya katika eneo lake kabla ya kufikiri kugombea zaidi nafasi hiyo.

Amesema kuwa, kuna baadhi ya watu ni ving’ang’anizi wa vyeo wakati nafasi hizo wanashindwa kuzitendea kazi na kuwa ufike wakati sasa kwao kujitafakari upya badala ya kuja kupata mshituko wa Moyo pale wanapoangushwa na wapinzani wao kwenye uchaguzi

“Mkae mkijua kuwa wapo watu huko nje wanahitaji kuingia ndani na nyie hamtaki kutoka hivyo kilichobaki sasa ni kujitafakari kwa kina kama mmetekeleza ipasavyo matakwa ya wananchi kama ambavyo ilani ya CCM inavyosema na wale mliokaa muda mrefu kwenye udiwani ondokeni kwa hiari mpishe na wengine wenye mawazo mapya,”amesema

Lakini pia alitoa siku saba kwa mkurugenzi mtendaji kuhakikisha kuwa wanawachukulia hatua kali wale wote waliohusika kuisababishia halmashauri madeni kwenye makusanyo ya ndani na kuisababishia halmashauri deni la sh.milioni 53.

Mwenyekiti wa halmashauri, Zeno Mwanakulya kwa upande wake amesema kuwa, ushauri wa mkuu wa mkoa ni vizuri ukazingatiwa na kuwa yeye mwenyewe binafsi anastaafu udiwani na hatagombea tena udiwani na kuwataka wenzie nao waliohudumu kwenye udiwani kwa mrefu waondoke na waingie wengine wenye nguvu mpya.

Amesema kuwa, hapendi kuona madiwani wenzie aliofanya kazi nao wakiadhirika kwenye uchaguzi na kuwa ukiona kabisa huna nafasi ya kushinda tena kwenye uchaguzi ujao ni vizuri ukaondoka kwa heshima na jamii itakutabua na itaendelea kukutumia katika shughuli nyingine za kimaendeleo.