Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa kutokana na utafiti mdogo uliofanywa na shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence maeneo ya ukanda wa ziwa ni maeneo hatarishi kwa watoto wa kike kufanyiwa vitendo vya ukatili.
Hayo yameelezwa na Ofisa Mradi wa kijana paza sauti chukua hatua kutoka shirika lisilo la kiserikali la Wadada Solutions on Gender Based Violence Elihaika Mugenyi, katika kikao na wadau mbalimbali kwa lengo la kuwakumbusha majukumu yao kilichofanyika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza kupitia mradi huo.
Ambapo mradi huo unatekelezwa Wilaya ya Ilemela katika Kata tano ikiwemo Sangabuye, Kitangiri,Shibula, Bugogwa na Kayenze ambao umewalenga vijana wenye umri kuanzia miaka 10-25 lengo ni kuwajengea uwezo katika masuala ya ukatili wa kijinsia,afya ya uzazi na stadi za maisha.
Amesema,awali waliweza kufanya utafiti mdogo na kubaini kwamba maeneo ya ukanda wa ziwa ambapo ndipo shughuli za uvuvi zinafanyika ni maeneo ambayo ni hatarishi sana kwa sababu mvuvi ni moja ya watu ambao wanaathiri sana watoto ambao wako shule kwa kuwalaghai,kuwapa pesa pamoja na usafiri.
Elihaika ameeleza kuwa,wanafahamu kabisa maeneo ya ukanda wa ziwa usafiri wa mwanafunzi wakati wa kwenda na kutoka shule siyo rafiki sana,hivyo inawalazimu wanafunzi wa kike kutembea umbali mrefu pindi wanapotembea wanaokutana na hao wavuvi ambao wanatumia fursa hiyo kuwalaghai.
“Tukaona sisi kama shirika tunajukumu la kufika maeneo hayo ambayo yapo mbali vijijini lakini pia kuzungumza na jamii ya wavuvi jamii ambayo bado inaishi katika zile mila na desturi kandamizi ambazo haziamini kabisa kwamba mtoto wa kike ana haki,hawajui kuhusiana na masuala mazima ya afya ya uzazi na ukatili unaotokea kwenye jamii,hivyo tuliguswa kupaza sauti zetu kwenye maeneo haya,” amesema Elihaika.
Awali akifungua kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Massala,amewataka wadau hao washirikiane kuibua changamoto zinazoendelea mitaani pamoja na kuendeleea kupaza sauti kwa matendo ya ukatili ambayo wakati mwingine yamekaliwa kimya huku watoto wanaathiriwa.
Massala amesema,mbaya zaidi hata wazazi wamekuwa sehemu ya kuvuruga utamaduni wetu ambapo wamepokea taarifa za baadhi ya wazazi kuwaingilia watoto wao na wanazo kesi ambazo zipo katika vituo vyao vya kisheria pia kuna shule ambazo zinafanya matendo hayo ambapo watoto wanaofanyiwa vitendo hivyo lakini walimu wapo kimya.
“Ofisi yangu,ofisi ya Mkurugenzi tunaendelea kupokea taarifa mbalimbali ambazo zinaendelea katika mitaa yetu,tunazo taarifa za watoto wetu wadogo kulawitiwa,pia kumekuwa na mimba za utotoni,watoto wanaacha shule haya yote kama jamii tunahitaji kujitafakari lakini kila mmoja anahitaji kuchukua hatua vitendo vya unyanyasaji kwa watoto wa kijinsia havikubaliki,sisi kama Wilaya ni miongoni mwa watu ambao tumeathirika sana kuhusiana na jambo hili,”ameeleza Massala.
Naye Mkurugenzi wa shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence Lucy John,ameeleza kuwa vitendo vya ukatili wakati mwingine vinatokea kwa sababu wazazi wengi hawakupata elimu ya ukatili wakati wanasoma.
Kwaio mikakati na malengo ambayo wamejiwekea ni kuona jamii ina kuwa salama ambapo wataendelea kutoa elimu katika maeneo yao ya kazi lakini shuleni na maeneo mbalimbali ili iweze kusambaa na watu wawe na taarifa sahihi ya ni wapi taarifa za msingi za ukatili wa kijinsia unaondelea katika jamii zao waweze kuripoti.
Naye mmoja wa wadau walioshiriki katika kikao hicho, Mtendaji wa Kata ya Shibula Petro Mwaisamila,ameeleza kuwa matumizi ya dawa za kulevya pamoja na ukosefu wa malezi chanya katika familia unachangia ukatili kutoishi kwenye jamii.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba