October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi Dismas Mbote ambaye ni Msimamizi wa Ujenzi wa Njia za maji pamoja na Bwawa kwenye Mradi wa Kufua Umeme kwa maji wa Julius Nyerere Mw 2115 akionyesha mashine aina ya Boring Mchine itakayotumika kuchoronga miamba katika eneo la lango la kupitisha maji kwenda kwenye mitambo ya kufua umeme,Mtambo huu ni wa kwanza kutmima Tanzania. Na Mpigapicha Wetu

Lango la kuingilia maji Mradi wa Nyerere kukamilika February

Na Mwandishi wetu

Msimamizi wa ujenzi wa njia za maji pamoja na bwawa kwenye Mradi wa Julius Nyerere, Mhandisi Dismas Mbote

UJENZI wa eneo la lango (Water Intake) la kuingilia maji kwenda kwenye mitambo ya kufua umeme katika Mradi wa Julius Nyerere (Mw 2115) unatarajiwa kukamilika Februari, 2022.

Msimamizi wa ujenzi wa njia za maji pamoja na bwawa kwenye Mradi wa Julius Nyerere, Mhandisi Dismas Mbote, amesema jana utekelezaji wa njia hiyo ulianza Oktoba, mwaka jana.

Ameongeza kuwa kazi ya uchimbaji wa lango imekamilika kwa kuchimbwa kina cha mita 53 ambapo hivi sasa kazi inayoendelea ni uondoaji wa kifusi na uchimbaji wa mahandaki matatu yatakayotumika kupitisha maji.

“Vifusi ambavyo vinachimbwa katika mradi huu wa Julius Nyerere havitupwi, mawe yanasagwa na kuwa mchanga, kokoto na mawe mbalimbali ambayo hutumika kwenye ujenzi”, amesema Mhandisi Mbote.

Aidha, amesema zitafanyika kazi za kuchoronga miamba pamoja na kuimarisha kuta kwa zege. Maji yatakayofua umeme kabla ya kwenda kwenye mitambo ya kufua umeme yataingia kwanza kwenye lango.

Pia amesema kwa hivi sasa imeletwa mashine ya kuchoronga miamba ambayo ni ya kwanza kwa Tanzania na inayotarajiwa kuongeza kasi katika uchimbaji wa mahandaki ya kupeleka maji kwenye mitambo.

Handaki la kwanza litakuwa na urefu wa mita 350, la pili mita 410 na la tano mita 570 hadi kwenye mitambo ya kufua umeme.