November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima wa kahawa washauliwa kupima afya ya udongo

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

IMELEEZWA   kuwa wakulima wa zao la kahawa wamekuwa wakishindwa kuzalisha kwa  tija kutokana na kutopima afya ya udongo ili waweze kujua ni mbolea gani inafaa na badala yake wamekuwa wakifanya  kilimo cha mazoea na wengine kutojua jinsi ya kuzuia magonjwa ya kahawa ,kutojua staili za kisasa za ukataji .

Kauli hiyo imetolewa jana Msimamizi mkuu wa shamba la kahawa Utengule Coffe  ,Amani Ngowi wakati wa siku ya mkulima ambapo wakulima mbali mbali walifika katika shamba hilo kupata kanuni bora za kilimo cha kahawa  kutoka kwa watalaam wa kilimo .

Ngowi amesema kuwa alichobaini ni kwamba wakulima wanashindwa kuzalisha kahawa kwa wingi kutokana na kutopima udongo ,kutokujua mbolea gani inahitajika na kufanya kilimo cha mazoea na wengine kutojua jinsi ya kuzuia magonjwa ya kahawa mashambani .

“Kuna magonjwa mengi yanatokea kwenye kahawa lakini wakulima wengi hawafahamu mfano mwaka jana ugonjwa wa hawa wadudu wadogo wadogo walitokea mwaka jana lakini wakulima hawafahamu ,tunashauri wakulima wapate elimu juu ya kilimo cha kisasa pia serikali iwasaidie wakulima wapate mbegu bora za kahawa  hii changamoto kubwa sana na hii itawasaidia wataweza kujikwamua kwenye kilimo mazoea na kwenda kilimo cha biashara”amesema Msimamizi huyo wa shamba .

Upendo Sailosi ni Mkulima kutoka utengule amesema kuwa kwenye kahawa kuna changamoto nyingi ambazo huwa wanatamani zitatuliwe lakini wakati mwingine zinatuliwa kiasi na zingine hazitatuliwi  hasa kwenye Kahawa ambapo  kuna wadudu ambao wanatoboa kwenye miti ya kahawa kahawa haiwezi kustawi tena  na mti huoza.

Mkulima huyo amesema kuwa siku ya mkulima huwa inakuwa msaada mkubwa kwani  kwani kuna mafunzo ambayo huwa yanatolewa  ambayo yana tija kwa mkulima ambapo hujifunza vitu ambavyo havijui na kumwongezea maarifa zaidi katika shughuli zake za kilimo .

Mkulima mwingine  wa Utengule Usongwe Peter Mwashitete amesema kuwa mafunzo hayo yamewasaidia namna ya kuotesha mbegu  kisasa na kupeleka shambani namna ya kukata miti ya kahawa pamoja na uchumaji  mpaka kuvundika .

Mwashitete amesema kwamba  Bodi ya Kahawa imewasaidia kupata mafunzo na usimamiaji mzuri wa zao kahawa Tanzania , ubora wa kahawa , minada ,bei ya kahawa  hivyo kwa wakulima msaada mkubwa sana.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda  ya Mbeya bodi ya Kahawa (TCB)Sijali Boa amesema kuwa lengo kubwa la siku ya mkulima  ni kuwaleta wakulima na wadau wengine kuwafundisha mbinu mbali mbali za kilimo cha kahawa ambapo mwisho wa siku tunategemea  wakizifuata  wazalishe kwa tija na kuongeza uzalishaji .

Boa amesema kuwa wamechagua shamba hilo kubwa la Kahawa la Utengule ili kuonyesha kuwa  wenzao wanafuata hatua zote za kilimo cha kahawa na wanazalisha kwa tija na kwa wingi lengo kubwa ni katika kuonyesha utofauti na kwamba wakulima wadogo wadogo waliopo pembeni mwa shamba  wanalima  na kufuata mbinu  bora za kilimo cha kahawa lakini hawazingatii kwa kiwango kinachotakiwa hivyo kushindwa kuzalisha kwa wingi .

Aidha amesema kuwa matarajio yao baada ya mafunzo hayo ni kuwataka wakulima kufuata mbinu bora za kilimo ili waweze kuzalisha kwa tija  na kupata kipato kikubwa zaidi.

“Pia tunatoa elimu kuhusiana  na masuala ya  afya ya udongo kimsingi unapokwenda kuzalisha sehemu yeyote lazima upime afya ya udongo  kwanza  ili kujua udongo uliopo kwenye mashamba yao unahitaji aina gani ya mbolea  hii itawafanya wakulima kujua aina ya udongo uliopo kwenye mashamba yao na kufahamu aina ya mbolea inayofaa kutumiwa”amesema Meneja huyo wa Kanda.

Msimamizi wa shamba la kahawa Utengule Coffe akitoa elimu kwa wakulima siku ya mkulima
Shamba la kahawa lililopo Utengule Usongwe
Mtalaam wa kilimo akitoa elimu kwa wakulima