Na Hadija Bagasha Tanga,
MKUU wa wilaya ya Muheza Mkoani Tanga Halima Bulembo amewatangazia vita wazazi wenye tabia ya kuwapa ajira watoto wadogo zikiwemo za uuzaji kashata, Mayai na karanga ambao wanapaswa kuwepo shuleni waache mara moja kabla hawajachukuliwa hatua kali za kisheria.
Amesema kwenye wilaya yake hataki kusikia wala kuona watoto wanaopaswa kuwepo shuleni wakihangaika mtaani kuuza bidhaa mbalimbali huku asisitiza wazazi na walezi kutambua kufanya hivyo ni kosa.
Kauli hiyo aliitoa wakati akihitimisha ziara ya kata kwa kata vijiji kwa vijiji aliyoifanya mara tu alipoteuliwa na Rais Samia kwenda wilayani humo ambapo lengo la ziara hiyo ni kujitambulisha kwa wananchi lakini pia kusikiliza kero na changamoto wanazokumbana nazo wananchi ili aweze kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
Akiwa katika ziara hiyo Mkuu huyo wa wilaya alisema alikutana na kesi nyingi za unyanyasaji wa watoto hivyo amesema wale wote wanaofanya hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ili kukomesha vitendo kama hivyo .
“Ajira kwa watoto wadogo ni kosa kisheria unakutana na mtoto amebeba kashata, mayai na karanga sasa ama zangu ama zenu nikikutana na mtoto anafanya hizo biashara nitamwambia anipeleke kwa wazazi wake na unakuta, ni muda wa shule lakini mtoto anauza kashata, kipindi cha wikiendi, sikukuu, su wamefunga shule watumeni mnavyotaka hata sisi tumekuwa hivyo wakati mwingine tukiwa likizo tunalima na kusaidia kazi za nyumbani lakini muda wa shule lazima aende shule, “alisistiza Bulembo.
Alibainisha kuwa watoto wengi wanaofanyiwa hivyo ni wale wanaoishi na mama zao wa kambo ama wa kufikia kwamba ndio wanaowanyanyasa hivyo amewataka kina mama kuacha tabia ya kunyanyasa watoto wao wa kufikia.
“Watoto wote wanatakiwa kupewa haki zao za msingi kama elimu, chakula na malazi lakini unakuta mtoto unamnyanyasa eti kisa ni mtoto wa mume wako kwani wakati mnapoenda kuolewa si huwa unaambiwa kuwa mume ana watoto wengine sasa kwanini uwanyanyase na waswahili wanasema ukipenda boga penda na ua lake sasa kwanini nyie ua lake hamlitaki, “ali7sema Bulembo.
Aidha amewataka wakazi wa Muheza kuwafichua wale wote wenye tabia ya kuwapa ujauzito watoto wa shule jambo ambalo limekuwa likikatisha ndoto za mabinti wengi.
“Mnawapa mimba sana watoto wa shule kwanini? Ukimpa mtoto wa shule mimba ni kosa kisheria unatakiwa uhukumiwe miaka 30 jela na si mimba peke ake hata ukiwa na mahusiano na mwanafunzi ni kosa kisheria sasa nyie mnawanyemelea kweli kweli sasa ni kwanini ni unifomu zao? Kama wanapendeza na unifomu zao wanunulieni na wake zenu wavae watoto wetu muwaache watimize ndoto zao, “alibainisha Bulembo.
Alisema matukio hayo yamekuwa mengi ambapo wakishawapa ujauzito wanafunzi wanakimbiloa mikoa mingine hivyo amebainisha kuwa atakayefanya hivyo na kuondoka basi atachukuliwa mzazi wake na kuwekwa jela hadi pale muhusika atakapopatikana huku akiwataka wazazi kuacha kumalizana kinyumbani pindi mtoto anapokuwa mjamzito.
Katika hatua nyingine Bulembo amemshukuru Rais Samia kea kuwapatia fedha ambazo zinakwenda kusaidia wananchi wa Muheza katika nyanja mbalimbali.
Alisema Halmashauri hiyo imepokea bilioni 7 kwajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, elimu, maji na barabara.
Sekta ya Afya imepokea bilioni 1.5 ambapo milioni 8 imepelekwa katika hospitali ya Wilaya ili kuongeza majengo mawili makuu ikiwemo chumba cha kuhifadhia miili, pamoja na jengo la mama na mtoto, wakati huo huo katika sekta hiyo wamepatiwa milioni 90 kwajili ya ujenzi wa nyumba tatu za watumishi wa afya.
DC Bulembo amesema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya maji ambapo kwa kuliona hilo Rais Samia amewapatia bilioni 1 kwajili ya sekta hiyo ya maji ambapo milioni 700 inakwenda kurekebisha miundombinu katika kata ya Kwemkabala, lakini pia wiki iliyopita wamepokea milioni 409 ambazo zitakwenda kuboresha miradi ya maji kwenye kata ya Masuguru na Tanganyika.
Wakati huo huo mkuu huyo wa wilaya amewasisitiza wakazi wa Muheza kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Halmashauri na badala yake amewataka waache kujiingiza kwenye taasisi zinatoa mikopo kwa riba huku wengine wakiishia kufilisiwa mali zao pamoja Samani za majumbani jambo ambalo amelilaani vikali
“Rais wetu mheshimiwa mama Samia anataka mpaja ifikapo 2025 wananchi wengi wawe wamenufaika na mikopo hii inayotolewa na Halmashauri zetu sasa mimi kinachonishangaza halmashauri ni yako hamtaki kukopa mnakimbilia kukopa barabarani wengi webu hapa mnafaiwa marejesho kweli sasa kwanini msiende kukopa kwenye fedha zisizokuwa na riba mikopo ya halmashauri ukikopa milioni 5 unarejesha hiyo hiyo, “amesisitiza Bulembo.
“Tuache kukopa kwenye watu wasiojulikana unachukuliwa Tv, unachukuliwa kitanda na kila kitu na ruba juu vijana hapa nawaona wengi wenzenu kule mitaani wanaendesha bodaboda sio kwamba wamenunua kwa fedha zao mkurugenzi na afisa mikopo wanajua tunawkopesha ni fedha za mama Samia kwahiyo na nyinyi changamkieni fursa badala ya kukaa vijiweni na kufanya mambo mengine tukajikwamue kiuchumi twendeni tukakope pale mikopo ni ya kila mtu, “amesisitiza DC Halima.
Mkurugenzi wa wilaya hiyo Nassib Mmbaga amesema watakaa pamoja na baraza la madiwani ili kuangalia namna ya kuondoa baadhi ya kodi katika machinjio yao baada ya wachinjaji wa nyama kudai kodi hiyo inasababisha kupanda kwa bei ya nyama.
“Tusifikiriakuipandisha tena nyama tutaingea na madiwani ili tuone ushuru gani unawabana tuuondoe ili kuwawezesha wananchi nao kupata kitoweo kulingana na hali zao tukiondoa tunataka kuona na nyama inashuka, “alisema Mmbaga.
Baadhi ya wakazi wa Wilaya hiyo wamempongeza Mkuu wa wilaya hiyo kwa kuweza kuwasaidia kutatua changanoto mbalimbali ambazo zilikuwa sugu hapo awali katika kipimdi kifupi alichokuwepo wilayani humo.
“Hakika mheshimiwa Rais hakukosea kukuleta Muheza tunasema tumepata jembe tumepata mtu anayesikiliza na kutatua kero zetu wana Muheza huu ni mfano wa kuigwa kwa viongozi wengine lakini pia mkuu wetu tunaomba uendeled kuwrka nguvu kubwa kwenye suala la maji bado kwetu ni tatizo kubwa, “amesema mmoja wa wananchi hao.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa