Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2020 zinaonesha kuwa takribani wanawake milioni 2 duniani wanaishi na ugonjwa wa fistula.
Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili na Tiba Mbadala kutoka Wizara ya Afya Dkt.Paulo Mhame katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kutokomeza ugonjwa wa fistula duniani,ambapo kitaifa yamefanyika mkoani Mwanza katika uwanja wa Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza.
Dkt Mhame ameeleza kuwa inakadiriwa wagonjwa wapya takribani 50,000 hadi 100,000 hupatikana kila mwaka wakati juhudi za kutibu fistula ulimwenguni kote huishia kutibu wagonjwa 20,000 tu ambapo wagonjwa hao zaidi wapo katika nchi za Afrika hususani Kusini mwa Jangwa la Sahara,Asia,nchi za kiarabu na Amerika Kusini.
Ameeleza kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na wanawake takribani 2500 ambao hupata fistula kila mwaka huku idadi ya wanaopata matibabu kila mwaka ni takribani wanawake 1,000 tu.
“Katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2016 hadi Desemba 2021,wanawake zaidi ya 5,500,wameisha tibiwa fistula na takwimu inaonesha wanawake wanaojitokeza kutibiwa katika vituo vinavyotoa huduma ya fistula ikiwemo CCBRT na Bugando imepungua kwa zaidi ya asilimia 30 ukilinganisha na mwaka 2015 na 2019 ambapo kwa mwaka 2015 idadi ya wanawake 1337 walipatiwa matibabu,mwaka 2016 wanawake 1356,2017 ni 1060,2018 idadi ilikuwa 900 huku 2019 ilishuka na kufikia idadi ya wanawake 852 hii inatokana na kuimarika kwa huduma za afya kwa mama wajawazito na hupatikanaji wa huduma za upasuaji za dharura,”ameeleza Dkt Mhame.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wanatakiwa kuwekeza vyema kwenye miundombinu ya afya ya huduma za ugonjwa wa fistula.
“Kauli mbiu ya mwaka huu ni “tokomeza fistula,wekeza,imarisha ubora wa huduma za afya na wezesha jamii ambayo ujumbe wake unaelekeza kila mtu na serikali kuhakikisha ugonjwa wa fistula unatokomezwa na wanawake wanaopata matatizo haya hawanyanyasiki kwenye jamii na haki za kupata huduma bora na kuhakikisha uwekezaji kwenye huduma za fistula nchini na watoa huduma kuzingatia utoaji bora wa huduma ya fistula kwa kuzingatia usawa,”ameeleza Dkt.Mhame.
Raisi wa Chama Cha Madaktari wanaofanya upasuaji wa fistula nchini,Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akina mama na upasuaji wa Fistula kutoka CCBRT,Daktari James Chapa, amesema ameeleza kuwa
mara nyingi wanawake waliokuwa wakipata fistula walikuwa wakitengwa na jamii na hata kukimbuwa na waume zao lakini kwa sasa jamii imepata elimu ndio sababu hata wanaume nao wanawapeleka wake zao ambao wamepata fistula hospital kupata huduma za afya na kuendelea kuonesha upendo kwao.
Mwakilishi wa shirika la UNFPA Felister Bwana,ameishauri serikali kupitia Wizara ya Afya kuboresha zaidi huduma za afya hasa kuchunguza vidokezo vinavyoweza kusababisha ugonjwa wa fistula pamoja na kuwa na mpango wa kuchunguza kama kuna dalili za mtu kupata fistula hii itasaidia kupunguza tatizo hilo.
“Wajawazito wanapimwa tu njia kama imefinguka ama anaweza kuzaa kawaida ila licha ya hivyo vyote kuonekana viko sawa lakini mgonjwa huyo anapata fistula wakati wa kujifungua,hivyo ni vyema Wizara kuwa na mpango wa kuchunguzwa dalili za mtu kupata ugonjwa huo,”ameeleza.
Kwa upande Mkurugenzi Mkazi wa shirika lisilo la kiserikali la Americares Tanzania Dkt. Nguke Mwakatundu,ameeleza kuwa moja ya huduma wanazozitoa ni pamoja na utoaji wa vifaa tiba katika vituo vinavyotoa huduma ya fistula ambapo limefanikiwa kuwasaidia wagonjwa 1700 kupata matibabu ya ugonjwa huo.
Naye Kiongozi Mtendaji Mkuu wa Kanda ya Ziwa kampuni ya mtandao wa simu wa Vodacom Ayubu Kalufya, ameeleza kuwa kama wadau wanashirikana kwa ukaribu tangu 2013 na CCBRT kuhakikisha wakina mama wanaweza kupata huduma za kiafya pindi wanapokuwa wajawazito ili wasiweze kupata ugonjwa wa fistula.
Mmoja wa wahanga wa ugonjwa wa fistula Neema Constantine,ameeleza kuwa baada ya kupata ugonjwa huo alikuwa anajinyanya hata yeye pamoja na kushindwa kujumuika na jamii katika shughuli mbalimbali ikiwemo misiba.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili