Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online
WAKILI Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),Nuru Maro amesema kuwa bado takwimu zinaonesha kuwa mazingira ya ufanyaji kazi kwa watetezi wa haki za binadamu nchini si rafiki na salama.
Pia amesema hali hii inatokana na mifumo na sheria zilizopo zinazowaongoza watetezi wa haki za binadamu bado si rafiki kwao katika utendaji kazi.
Akizungumzia hayo leo jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 10 ya mtandao wa watetezi wa haki za binadamu nchini alisema mpaka sasa Tanzania bado haijaridhia Mkataba wa Kimataifa wa Watetezi wa haki za binadamu hivyo kufanya watetezi hao kutokuwa na ulinzi thabiti wakati wa utendaji kazi.
“Ndio maana sasa tunatoa maoni yetu kwa serikali iweze kuridhia mkataba huu wa mwaka 1998 ili watetezi wa haki za binadamu waweze kulindwa kisheria, na waweze kufanyakazi katika mazingira salama zaidi,”amesema na kuongeza
“Kuna changamoto nyingine ya viongozi wa wilaya, mikoa na kitaifa, kudharau kazi hii na kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watetezi wa haki za binadamu, hivyo tunaiomba Serikali iweze kuboresha mashirikiano baina yao na wadau hawa kwa ajili ya manufaa ya watanzania na nchi kwa ujumla,” amesema.
Amesema katika kuadhimisha miaka10 ya mtandao huo kumekuwa na matokeo makubwa ikiwemo ya watetezi wa haki za binadamu kujitambua, serikali kutambua mchango unaotolewa na watetezi hao katika maendeleo ya taifa.
“THRDC imekuwa ikishirikiana na Serikali kwa ukaribu kwa sasa ilinganishwa na miaka ya nyuma, huko nyuma serikali ilikuwa haijatambua umuhimu wa watetezi wa haki za binadamu katika maendeleo ya taifa,” amesema na kuongeza
“Kama mtandao tutaendelea kuboresha hali ya haki za binadamu ili watetezi waendelee kuwasaidia watanzania katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili waweze kushiriki katika shughuli za kimaendeleo,” amesema
Naye Mratibu wa THRDC Kanda ya Mashariki na Pwani, Michael Marwa amesema miaka ya nyuma mahusiano ya watetezi wa haki za binadamu na taasisi za serikali hayakuwa mazuri na hiyo ni kutokana na kukosekana kwa uelewa juu ya kazi zinazofanywa na watetezi wa haki za binadamu
Marwa amesema ndani ya miaka 10 kwa tathimini waliyoifanya jana, leo na kuendelea kesho wameona kwamba uhusiano huo umeimarika na hiyo inadhihirika zaidi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi