November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Nape atoa siku 14 kwa Maafisa Habari nchini kuhakikisha tovuti ya serikali na mitandao ya kijamii iwe na taarifa zinazoendana na wakati

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Waziri wa habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ametoa siku 14 kwa maafisa habari nchini kuhakikisha kila tovuti ya serikali na mitandao ya kijamii iwe na taarifa zinazoendana na wakati huku akiahidi kuwashughulikia maafisa habari watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo.

Pia waziri Nape amewataka maafisa habari wa serikali wasiruhusu watu wapotoshe mafanikio ya serikali na badala yake wametakiwa kujibu hoja ili kuwaelewesha wananchi.

Waziri Nape ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa akifungua kikao cha 17 cha maafisa habari, mawasiliano na uhusiano wa serikali kinachoketi kwa siku tano jijini Tanga.

Awali akifungua kikao hicho Waziri Nape amesema kumekuwa na tatizo sugu la muda mrefu katika tovuti na mitandao ya kijamii za wizara na taasisi mbalimbali za serikali kuwa na habari zilizopitwa na wakati.

“Nitoe siku 14 kuanzia tarehe 14.5 kila tovuti ya serikali au taasisi ya serikali au serikali za mitaa iwe na taarifa zinazoendana na wakati afisa habari atakayeshindwa kutekeleza hili ndugu Msigwa hatutaweza kuendelea naye inabidi tuachane naye, “amesema Waziri Nape.

Aliongeza kuwa najisikia vibaya sana ninapopita na kusikia kuna taasisi za serikali tovuti za Mkoa za wizara, Wilaya au Halmashauri zina taarifa za miaka miwili au mitatu iliyopita halafu tuna afisa habari kwenye hilo eneo haiwezekani jamani na tusipoambiana tutakuwa hatutendeani haki jamani sasa siku 14 zinatosha kabisa Msigwa ulikague na nipate taarifa ya jambo hili.

Ameongeza kuwa nasikitika kuona tovuti ya wilaya, Mkoa, Halmashauri haziendani na wakati watu wengi wameacha kutembelea tovuti za serikali kwajili ya kuwepo taarifa zilizopitwa na wakati tutoke kwenye aibu hiyo tumewafanya watu hawatembelei tovuti za serikali halafu tuna afisa tena anajiita afisa habari, “amesisitiza Waziri Nape.

“Mhakikishe mnajibu hoja za wananchi kwenye vyombo vya habari kwa wakati muafaka kuhusu changamoto zinazojitokeza msiruhusu watu wapotoshe ukweli kwani ukweli unapopotoshwa ni aibu kwa maafisa habari supu inanywewa ya moto usisubiri mpaka usukumwe kwenda kukanusha habari ambayo ni ya uongo akikibu saa moja saa mbili nawe sema tukiends hivyo watakuwa na nidhamu kwenye kupotosha, “alisistiza Waziri Nape.

Aidha Waziri Nape ameagiza utengenezwe utaratibu wa mafunzo kwa maafisa habari nchi nzima juu ya miradi mikubwa ya kitaifa inayotekelezwa na serikali ili wawe na uelewa wa kuisemea miradi hiyo wakati wowote.

“Sote tunafahamu katika mwaka mmoja wa Rais Samia ameleta mageuzi makubwa ambayo tumeyashuhudia jukumu letu ni kuhakikisha Lengo la kufanya hivi ni kwamba tunataka kila afisa habari hata anapoamshwa usingizini awe anaijuanikiamini tukifanya hivyo tutawapa uwezo wa kitu cha kusema, “amebainisha waziri Nape.

Waziri Nape amesema kwenye Mikoa na Wilaya masfisa habari wa eneo husika wachukue muda wa kuelewa miradi inayoendelea kwenye maeneo yao ili wawe na jambo la kusema akitolea mfano Mkoa wa Tanga ujenzi unaoendelea wa kuwahamisha watu wanaotoka Ngongoro kuja Msomera afisa habari wa Tanga na maeneo yale wanapaswa kufahamu kwa kina kinachoendelea.

Aidha ameagiza iandaliwe mijadala ya maafisa habari kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kupunguza gharama kubwa kwa kufanya majadiliano ya pamoja kupitia teknolojia jambo ambalo amesema linawezekana.

Katika hatua nyingine Waziri Nape ameahidi kupeleka mara moja maafisa habari katika Mikoa 7 inayokabiliwa na ukosefu wa maafisa habari ikiwemo Mikoa ya Manyara, Lindi, Mbeya, Tabora, pamoja na mikoa ya Kigoma, Dodoma na Geita ambayo maafisa habari wske wamekuwa wasaidizi wa wakuu wa mikoa.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa wizara ya habari Jimmy Yonazi amesema tansinia ya mawasiliano kwa umma ni ya zamani na ni muhimu kwasababu ndio imeandika historia ya serikali juu ya namna inavyohudumia wananchi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kimaendeleo.

Katibu mkuu huyo amemshukuru Rais Samia kwa kuifanya sekta hiyo kuwa pamoja na kupelekea kuwezesha taarifa kuwafikia wananchi jambo hilo linatoa taswira mpya lakini kutoa msukumo mpya na muelekeo mpya kwa maendeleo nchini.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha katibu Mkuu Mkurugenzi wa idara ya habari maelezo na msemaji mkuu wa serikali Grerson Msigwa amesema kuwa ni heshima kubwa aliyopewa na Rais na hivyo wana deni kubwa la kulipa kwa kufanya kazi bila kuchoka usiku na mchana kwa kuzingaia uadilifu, ubunifu, na mabadiliko yanayotokes kila uchwao katika sekta hiyo nchini.

“Tokea nimeteuliwa na mheshimiwa Rais kuwa Mkurugenzi wa idara ya habari maelezo nimshukuru Mheshimiwa Waziri na katibu mkuu kwa kuwa wameweza kunishika mkono na kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu kwa ufanisi bila vikwazo vyovyote, “alisistiza Msigwa.

Mwenyekiti wa maafisa habari Nchini Pascal Shelutete alimshukuru waziri kwa kuwa mgeni rasmi katika kikao hicho huku akiahidi wao kama maafisa habari wa serikali hotuba ya Waziri ni maelekezo hivyo katika siku 5 watakazokuwepo jijini Tanga watahakikisha wanaweka mikakati madhubuti ya kuyafanyia kazi maelekezo yote.