November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Li-TAFO yaomba wadau kuchangia ujenzi kituo cha kutolea huduma kwa wenye usonji

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa kukosekana kwa kituo cha usonji Kanda ya Ziwa ni moja ya changamoto kwa watoto na vijana wenye usonji mkoani Mwanza,hali inayosababisha gharama kubwa pamoja na kufuata huduma mbali.

Hivyo wito umetolewa kwa wadau na jamii kwa ujumla kuunga mkono jitihada za taasisi ya Living Together Foundation (Li-TAFO),kwa kuchangia gharama za ujenzi wa kituo kwa ajili ya huduma za usonji katika Mkoa wa Mwanza.

Hayo yameelezwa na Volunteer wa Li-TAFO James Mushi,wakati akisoma risala ya kilele cha maadhimisho ya siku ya usonji duniani, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, yalioandaliwa na Li-TAFO yaliofanyika mkoani Mwanza.

James ameeleza kuwa,kupitia uzoefu wao katika kutoa huduma na kushughulika na masuala ya usonji wamebaini kuwa Kanda ya Ziwa wamekuwa na idadi kubwa ya watoto na vijana wenye changamoto ya usonji.

Pia uelewa kwa jamii juu ya kushughulikia changamoto hiyo umekuwa mdogo sana ambapo huduma za usonji wamekuwa wakizifuata mbali ikiwemo Moshi na Dar-es-Salaam ambalo kuna vituo mahususi kwa ajili ya suala hilo.

Amesema,baada ya kujengwa na kukamilika kwa kituo hicho wanatarajia kitatoa huduma za masuala ya usonji katika afya,mazoezi ya tabia, vitendo na kuzungumza,elimu na ushauri kwa wazazi, walezi na jamii.

Kwani shule nyingi jumuishi hazina mazingira rafiki ya kukidhi mahitaji ya watu wenye usonji huku wakipongeza juhudi za serikali ya Mkoa kuwakubalia kuwapatia kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ambapo suala hilo bado lipo kwenye mchakato na wanaendelea kufuatilia.

“Tunaomba mgeni rasmi kutilia mkazo suala la kupatiwa kiwanja na wadau pamoja na jamii kutushika mkono kwa kuchangia gharama za ujenzi wa kituo hiki ili watoto waweze kupata huduma karibu na kupunguzia gharama wazazi na walezi kama ilivyo sasa wanafuata huduma hizo mbalimbali ambapo mpaka kukamilika kwa kituo kitagharimu kiasi cha milioni 699.3,”amesema James.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli, amesema ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza haitakuwa kikwazo katika kuwapatia kiwanja ili kuhakikisha wanawahudumia watoto wenyewe usonji.

“Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,wakuu wa Wilaya zote saba na wadau,tutashirikiana na wewe Mkurugenzi wa Li-TAFO Injinia Shangwe Mgaya kuhakikisha ujenzi wa kituo hicho unafanikiwa,ni sehemu ya serikali kuhakikisha tunasaidia watoto wenyewe usonji waweze kuishi kama watoto wengine na wana haki sawa kama watoto wengine,” amesema Kalli.

Daktari Bingwa wa mfumo wa ubongo na mishipa ya fahamu wa hospitali ya Saifee,Dkt Yusuf Jamnagerwalla, amesema usonji unasababishwa na kupooza kwa ubongo au mwili shida ambapo shida iliopo ni uelewa wa jamii hasa katika kutambua dalili za awali za usonji ambapo kwa wazazi walio makini watagundua dalili za usonji mtoto akifikisha miezi sita.

Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Sebastian Kolowa Memorial (SEKOMU) Alfred Walalaze amesema,kumekuwa na mitazamo hasi kwa jamii ambayo inamchukulia mwenye usonji au ulemavu wa akili kama mzigo na mtu asiyestahili kupatiwa huduma muhimu kama wengine.

Hivyo amesema,ili kuondoa changamoto zinazowakabili wenye usonji kuwapatia elimu wazazi na jamii kwanza kukubali kuwa ulemavu huo ni mapenzi ya Mungu na kuwaelekeza mahali pa kupata msaada ikiwemo vituo vya afya,shule na hospitali.

Pamoja na kuwashirikisha watoto hao kwenye mambo ya msingi pamoja na kujitambua pia wawafundishe kujitegemea kwa mambo ya msingi yanayowagusa moja kwa moja,kutomficha ndani badala yake wawapeleke shule pamoja na kuwapatia haki zao msingi kama wengine.

Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli,wa pili kushoto akimkabidhi mmoja wa wazazi wenye watoto wenye tatizo la usonji kitabu kwa ajili ya kuwafundishia watoto wenye changamoto hiyo,katika hafla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya usonji duniani iliofanyika mkoani Mwanza na kuandaliwa na taasisi ya Li-TAFO huku wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Injinia Shangwe Mgaya.(picha na Judith Ferdinand)
Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli, akizungumza katika hafla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya usonji duniani iliofanyika mkoani Mwanza na kuandaliwa na taasisi ya Li-TAFO.(picha na Judith Ferdinand)
Daktari Bingwa wa mfumo wa ubongo na mishipa ya fahamu wa hospitali ya Saifee Dkt.Yusuf Jamnagerwalla, akizungumza katika hafla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya usonji duniani iliofanyika mkoani Mwanza na kuandaliwa na taasisi ya Li-TAFO.(picha na Judith Ferdinand)
Volunteer wa Li-TAFO James Mushi,akisoma risala ya kilele cha maadhimisho ya siku ya usonji duniani, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli( hayupo pichani) ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, yalioandaliwa na Li-TAFO yaliofanyika mkoani Picha na Judith Ferdinand
Baadhi ya wazazi na watoto waliohudhuria katika hafla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya usonji duniani iliofanyika mkoani Mwanza na kuandaliwa na taasisi ya Li-TAFO.picha na Judith Ferdinand