November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yataja sababu ya kufanya marekebisho ya Katiba ya Chama chao

Na Penina Malundo, TimesMajira,Online

CHAMA  cha Mapinduzi (CCM), kimesema sababu ya kufanya marekebisho ya katiba ya Chama chao   ni pamoja na kuongeza kasi ya ufanisi wa kazi za chama na utekelezaji wa maamuzi ya vikao vya chama.

Akizungumza leo na waandishi wa habari, Katibu wa Itikadi na Uenezi  Shaka Hamdu Shaka katika Ofisi ndogo za Makao Mkuu jijini Dar es Salaam amesema Kamati Kuu imepokea na kujadili pendekezo la kuitishwa kwa mkutano mkuu maalum wa CCM Taifa.

Amesema pia lengo la marekebisho ya katiba hiyo lengo ni  kuongeza na kuimarisha udhibiti wa chama na viongozi wake wanaochaguliwa na kuongoza kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM kupiti Serikali za mitaa.

“Pia tunataka kuimarisha nguvu za chama katika kukabiliana na kudhibiti vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka, kuongeza jumuiya za chama ngazi za kata kwenye mkutano mkuu wa CCM Wilaya, na kurekebisha itifaki za uwakilishi unaofanana wa wenyeviti na makatibu wa jumuiya ngazi za mikoa kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wa Taifa na ngazi za Wilaya kuwa Wajumbe wa mkutano mkuu wa Mkoa,”amesema

Shaka amesema  mamlaka ya kupitisha na kurekebisha katiba ya hiyo, yapo mikononi mwa mkutano Mkuu Chini ya ibara ya 99 (5) ya katiba ya chama ya mwaka 1977 toleo la 2020.

“Kamati Kuu ya  Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imeazimia kuwasilisha kwa Halmashauri Kuu Taifa pendekezo la kuitishwa kwa mkutano mkuu maalum wa CCM  Taifa” amesema.

Akitaja ratiba za vikao amesema, Machi 31,2022 Kamati Kuu ya CCM itakutana na kufuatiwa na Halmashauri Kuu ya Taifa siku hiyo hiyo.

“Aprili Mosi,2022 Mkutano Mkuu Taifa utafanyika na vikao vyote vilivyotajwa vitafanyika Makao Makuu Dodoma,” amesema na kuongeza.

“Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu katika kikao chake kilichokutana Machi 11, 2022 Jijini Dodoma chaji ya mwenyekiti Rais Samia Suluhu kimepitisha mpango wa chama kuhusu maadhomisho ya kumbukizi ya kitaifa ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa baba wa Taifa hayati mwalimu Julius Nyerere,”amesema 

Aidha amesema  mwaka huu chama kitaadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa kiongozi mahiri, mzalendo na mwanamapinduzi wa kweli.

“Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu imedhamiria na kieleleza kufanyika kwa mdahalo wa kitaifa ambao utakumbushia mena na mazuri kwa kuzingatia tulipotoka, tulipo na tunapoelekea huku tukitafakari kama Taifa namna ambavyo tunaendelea kuishi katika nadharia za kiongozi wetu mashuhuri Mwalimu Nyerere,”amesema Shaka 

Amesema mdahalo huo unatarajiwa kufanyika  Aprili 9,2022 katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Kibaha na kuhudhuriwa na wanazuoni wa Siasa, Uchumi, uongozi na utawala pamoja na watu waliofanya kazi na Mwalimu Nyerere.