December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

THRDC wakutana na Waziri Simbachawene

Na Penina Malundo,timesmajira,Online

WADAU kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC, wametembelea Wizara ya Katiba na Sheria na kukutana na Waziri George Simbachawene na kuzungumza mambo mbalimbali ikiwemo kuundambulisha Mtandao huo na kutoa maoni mbalimbali ambayo Wizara hiyo ingeweza kufanya maboresho.

Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo, Mratibu wa kitaifa wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa amempongeza Waziri Simbachawene kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo, huku akiutambulisha mtandao na kutoa baadhi ya mapendekezo ya mtandao huo katika kuboresha mashirikiano baina yake na serikali kupitia wizara hiyo.

Amesema hadi mtandao wao una wanachama zaidi ya 200 waliogawanyika katika kanda 11 nchini ambao hufanya kazi katika maeneo yote ya haki za binadamu, ikiwemo maeneo ya wanawake, pamoja na watoto huku wanachama hao wamekuwa wakishirikiana na wizara ya katiba na sheria pamoja na wizara ya jinsia na watoto, maeneo ya elimu, afya, amani, pamoja na utoaji wa msaada wa kisheria.

Olengurumwa amesema kuwa baadhi ya maeneo muhimu ambayo AZAKI zimekua na mchango wa moja kwa moja kwa Serikali ni pamoja na eneo la utoaji wa huduma za afya, usafi wa mazingira, maji, ambapo kulingana na uchambuzi uliofanywa na serikali katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa (FYDP III), AZAKi zimekuwa zikichangia asilimia 40 ya uwekezaji katika sekta ya afya.

Baada ya hoja mbalimbali kuwasilishwa na THRDC,Waziri Simbachawene amefurahishwa na ujumbe uliomtembelea ambao umezingatia usawa wa kijinsia pamoja na kujumuisha Wadau kutoka pande zote za muungano.

“Naipongeza hatua iliyochukuliwa na wadau wa sekta ya AZAKI katika kuona umuhimu wa kukutana na wizara na kuwasilisha mapendekezo hayo kwa malengo ya mashirikiano huku akiwakaribisha wadau wengine kujtembelea wizara hiyo kwa malengo ya mashirikiano,”Amesema Waziri Simbachawene

Waziri Simbachawene amesema Tanzania ni nchi ambayo inatambua, inaheshimu, inatunza na kulinda Haki za binadamu, hivyo wao kama wizara watashirikiana na taasisi hizo za wadau wa Haki za Binadamu na katika kazi nyingi wanazozifanya kwani zinasaidia Serikali.

Amesema katika mwaka mmoja wa uongozi wake, Rais Samia amedhihirisha nia ya kutanzua maeneo ambayo yameonyesha kuwa na shida katika eneo la Haki za Binadamu na amekuwa akifanya hivyo kwa vitendo, na nadharia, huku akiahidi mashirikiano zaidi ya wizara yake na wadau wa Haki za binadamu nchini.

“Wizara ya Katiba na sheria imefurahi kuona mpo na itaendelea kushirikiana na nanyi katika kila jambo ambalo mtapenda tushirikiane.” Waziri Simbachawene

Waziri Simbachawene amewataka watetezi wa Haki za Binadamu nchini kuhoji na kuzungumza na wizara pale kunapotokea jambo lenye ukakasi katika serikali, badala ya kupeleka hoja katika majukwaa ya kimataifa na kuiondolea heshma nchi. Ameeleza kuwa Nchi ya Tanzania ndio mama yetu hivyo inapaswa kujengwa kwa ushirikiano.