November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAC wataka urasimishwaji wa bandari bubu

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Shirika la uwakala wa meli Tanzania (TASAC) kapteni Mussa Mandia ameishauri mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania TPA kuangalia uwezekano wa kurasimisha bandari bubu zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini ili kurahisisha utoaji wa huduma.

Hatua hiyo inaweza kusaidia udhibiti wa biashara za magendo ambazo zimekuwa zikiingia kupitia bandari bubu kufuatia wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi.

Mwenyekiti huyo ametoa kauli hiyo kwenye ziara ya kutembelea mradi mkubwa wq ujenzi la gati la kisasa katika bandari ya Tanga.

Kapteni Mandia amesema kuwa urasimishaji wa bandari hizo utasaidia kuongeza mapato kwa Halmashauri husika sambamba na Bandari yenyewe.

Akizungumzia kuhusu upanuzi wa bandari ya Tanga Kapteni Mandia amesema kukamilika kwa ujenzi wa gati la kisasa katika bandari ya Tanga kutasaidia kuongeza ufanisi na usalama kwenye bandari hiyo.

“Tumekuja kutembelea bandari za Tanga siyo ya Tanga bali za Tanga kwamaana ya bandari kubwa na bandari ndogo kama mnavyojua Tanga kulikuwa na bandari bubu nyingi na tuliwahi kutoa maelekezo siku za nyuma kwa wenzetu wa TPA warasimishe bandari ili wapunguze kwa manufaa ya Taifa, “

Kapteni Mandia amesema suala la ulinzi na usalama limeanzia kwenye bandari kubwa ya Tanga ambayo historia inawaambia bandari hiyo ilianza kujengwa kwa mara ya kwanza mwaka 1888 na kuisha mwaka 1891 ambapo hivi sasa wanashuhudia kazi inatoendelea ya uboreshaji wa bandari hiyo kwa lengo la kuimarisha operesheni za bandari hiyo ili kuweza kubeba mizigo mingi zaidi kwa njia ya kiusalama.

Mwenyekiti huyo wa bodi amesema kazi yao pia ni kusimamia usalama wa bandari pamoja na utendaji wake ambapo hivi sasa katika bandari ya Tanga panafanyika kazi ya kuongeza kina cha bandari ili kufikia mita 13 kutoka mita tatu zilizokuwepo hapo awali.

Kapteni Mandia amesema uongezwaji wa kina katika bandari hiyo kutasaidia kuruhusu meli kubwa kuingia bandarini kwani hapo awali operesheni zilikuwa zinafanyika katikati ya maji lakini hivi sasa baada ya kazi hiyo ya ujenzi wa gati hilo wanatarajia mpaka mwezi octoba bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa bandarini hapo.

Kwa upande wake meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha amesema ujenzi huo wa gati linakwenda sambamba na masuala ya kiusalama ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kufuatia meli nyingi zitakazotia nanga kwenye bandari hiyo baada ya gati hilo kukamilika.

Meneja Mrisha amesema mradi utakapokamilika utasaidia kuingiza meli kubwa ikiwemo za magari ambazo hazijawahi kutia nanga kwenye bandari a Tanga.

Meneja huyo alisema hivi sasa bandari ya Tanga inahudumia Tani laki saba kumi na nane na mianne lakini gati hizo mbili zitakapokamilika bandari hiyo itakuwa na, uwezo wa kuhudumia mpaka Tani milioni 3.

Ujenzi huo wa gati mbili una urefu wa mita 450 na matarajio ni kwamba ifikapo mwezi mei mwaka huu mita 150 zitakuwa zimekamilika na kuanza kupokea meli zisizozidi urefu huo wa 15 na mwezi octoba mita 450 zote zitakuwa zimekamilika.