November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Bashungwa alitaka Shirika la Elimu Kibaha kuwa na mipango mikakati ya kiuchumi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

UONGOZI wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) umetakiwa kuwa na mipango mikakati ya kiuchumi ili kuliwezesha kupiga hatua na kuachana na baadhi ya mipango ambayo imepitwa na wakati.

Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Innocent Bashungwa ameyasema hayo alipotembelea kuona baadhi ya miradi inayoendeshwa na kujua uendeshaji wa shirika hilo.

Bashungwa amesema kuwa, shirika hilo ni moja ya mashirika makongwe nchini, hivyo lazima liwe na mipango inayoendana na wakati.

Amesema miradi kama ya shule inafanywa kila mahali hivyo ni bora wakaja na mipango ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo vijana wanaokosa nafasi za kwenda kidato cha tano na wale wanaomaliza vyuo vikuu.

Ameongeza kuwa, katika kufanikisha mipango hiyo timu kutoka TAMISEMI itaungana na wataalamu wa shirika ili kuibua mipango ambayo itawapatia fedha na kubuni vyanzo vya uzalishaji mali na mapato.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, Robert Shilingi amesema kuwa shirika hilo mbali ya kupata baadhi ya mafanikio lakini kuna changamoto ambazo zinalikabili ikiwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu ambayo imejengwa zaidi ya miaka 60 iliyopita.

Shilingi amesema kuwa, changamoto nyingine ni mchakato wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi ambayo iko chini ya shirika hilo kwenda Wizara ya Afya ambapo watumishi kutokana na miundo wanashinda kupandishwa vyeo kutokana na kutumikia sehemu mbili kwa wakati mmoja.

Amesema, wanaishukuru serikali kupitia mradi wa fedha za shule kongwe ambapo wao walipata fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.1 ambapo ukarabati umeufanya shule ya sekondari Kibaha kuwa kwenye mazingira mazuri.

Naye mwanafunzi wa shule ya Kibaha sekondari Abdulkarim Masa alisema kuwa wanatoa ahadi ya kufanya vizuri ambapo wanamuahidi kuwa watapata daraja la kwanza tu na hakuna mwanafunzi atakayefeli.

Naye Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Tumbi Robert Jani alisema kuwa,wanaishukuru serikali kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vitatu.