November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Jafo atoa siku 14 Kinondoni kurekebisha mfumo wa maji taka

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo ametoa muda wa siku kumi na nne kwa Uongozi kwa Wilaya ya Kinondoni kuhakikisha wanatatua tatizo la mfumo wa majitaka katika Mtaa wa Ufipa, Dar es Salaam.

Dkt. Jafo ametoa agizo hilo leo 25/02/2022 baaada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Mtaa wa Ufipa na kujionea uharibifu mkubwa wa mazingira utokanao na mfumo wa maji taka ambao miundombinu yake imeharibika na kutiririsha maji taka katika makazi ya watu.

Akiwa katika eneo hilo Dkt. Jafo amesikitishwa na maelezo ya wataalamu wa DUWASA, TARURA na Manispaa ya Kinondoni kutokuwa na habari ya changamoto inayowakabili wakazi wa eneo la Ufipa.

“Wataalamu msikae Ofisini tu, tokeni mje msikilize na kutatua kero za wananchi, haiwezekani mimi Waziri wa Mazingira nitoke Dodoma kuja kukagua na kuleta ufumbuzi wa tatizo hili wakati ninyi mpo hapa kila siku” Jafo alisisitiza.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Godwin Gondwe amesema atahakikisha tatizo hilo linapatiwa ufufumbuzi ndani ya siku 14 kama Waziri Dkt. Selemani Jafo alivyoelekeza.

“Mhe. Waziri nikuhakikishie, sisi Wilaya ya Kinondoni kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi, siku ya Jumatatu yaani 28/02/2022 tutawasilisha kwako mpango kazi wa utekelezaji katika kutatua suala hili” Gondwe alifafanua.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa eneo hilo Rajab Juma amesema changamoto hiyo ya majitaka katika makazi yao ni ya muda mrefu na imekuwa ni kero hususan kipindi cha mvua ambapo majitaka hufurika na kuhatarisha usalama wa maisha yao pamoja na kukabiliwa na mlipuko wa magonjwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo akimsikiliza Rajab Juma Mkazi wa Ufipa akielezea changamoto wanayoipata katika makazi yao kutokana na mfumo wa majitaka usio rafiki kwa mazingira. Dkt. Jafo ametoa muda wa siku 14 kwa Uongozi wa Wilaya ya Kinondoni kutatua tatizo hilo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Godwin Gondwe
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Wilaya ya Kinondoni kutatua kwa haraka tatizo la mfumo wa maji taka unaopita katika makazi ya watu ambao miundombinu yake imechakaa na kusababisha kero kwa wakazi wa Mtaa wa Ufipa. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe.
Picha ikionyesha mfumo wa maji taka unaopita katika makazi ya watu pia miundombinu yake imechakaa na kusababisha kero kwa wakazi wa Mtaa wa Ufipa ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo ameagiza eneo hilo la Ufipa kupatiwa ufumbuzi mapema.