Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wazazi ambao watoto wao wametoroka majumbani kuwarudisha haraka kabla hatua kali za sheria hazijachukua mkondo wake.
Wito wa kuchukua hatua hiyo utafuatiwa na mikakati ya kuwaondoa watoto wa mitaani na kuwapeleka katika vituo maalum kwa mafunzo huku wale walioathirika na uvutaji wa bangi, gundi na petroli wakipelekwa katika matibabu kwenye vituo vya kurejesha waraibu.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo leo Februari 24, 2022 mkoani Dar es Salaam wakati wa ziara yake aliyoifanya katika shule ya msingi Mbutu iliyopo eneo la Gezaulole, Kigamboni alipofika kukagua kituo cha kulelea watoto wadogo kilicho chini ya programu ya malezi na makuzi jumuishi kwa maendeleo ya awali watoto.
“Serikali katika kulifanyia kazi hilo, imeshatoa nafasi kwa wadau kusaidiana kwa pamoja ili kuondoa wimbi la watoto waliopo mitaani kupitia mkakati wa pili ulioanza kutumika Juni 2020,
“Wakati hilo linafanyika nimewaagiza maafisa maendeleo ya jamii na ustawi wakati tunapambana na wa mitaani, waliopo majumbani pia tuwaangalie hasa wale wanaoishi katika mazingira hatarishi,” alisema.
Aidha Waziri Gwajima alitoa wito kwa wazazi wasiowajibika huku akisema watoto walio mitaani ni matokeo ya wazazi wasiowajibika, ingawaje wapo yatima na watoto watukutu na kwamba taarifa ya uchambuzi itabaini ni wazazi kutowajibika au kosa la mtoto na hatua zitachukuliwa.
“Mzazi unayejua mtoto wako yupo mtaani mrejeshe usisubiri Serikali imtafute na kumrejesha, ili wote tuongee lugha moja,” alisema.
Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima alisema programu ya makuzi jumuishi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto imeanza kufanya kazi baada ya maandalizi ya vituo 30 mkoani Dar es Salaam na Dodoma kukamilika.
Alisema programu hiyo ina lengo la kumlinda mtoto, kumlea na kumkuza apate malezi ambayo yatamfanya akue katika mfumo uliomwandaa kuwa bora kabla hajaanza rasmi shule.
“Mradi wa makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto umeanza kwa vituo 30 Dar es Salaam vipo 10 na Dodoma vimejengwa 20. Vituo hivi vitajengwa nchi nzima, lengo ni kuwawezesha wazazi kufanya kazi lakini pia ulinzi kwa mtoto na kumjenga kiakili kabla hajaanza shule” alisema Dkt. Gwajima.
Hili pia ni mojawapo ya yaliyopo kwenye Mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) na utekelezaji wa mpango huo ni kupunguza ukatili miongoni mwa wanawake na watoto kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.
Kwa upande wake Mwalimu Mlezi wa Kituo hicho cha Mbutu, Zubeda Mohamed alisema watoto wanapewa mafunzo mbalimbali ya stadi za kuimarika kimwili pamoja na michezo mbalimbali ya kuwajenga na kuwakuza miili, mifupa na akili zao.
“Kuna kona ya ubunifu inayomjenga mtoto awe mbunifu na kipawa chake anakuwa na udadisi, ubunifu, kona ya rangi inamsaidia kujua rangi zote na hata nguo aliyovaa ina rangi gani, kona ya muziki inamsaidia pia, kona ya michezo halikadhalika,” alisema Mwalimu Zubeda.
Ameongeza kuwa kituo hicho kilichofunguliwa rasmi Januari 17, kina watoto 40 ambapo wakike ni 21 na wa kiume 19 na kwamba mzazi hulazimika kutoa kiasi cha Sh20,000 kwa ajili ya uji na chakula cha mchana kwa mwezi.
Mmoja wa mkazi wa Mkwajuni Simon Joseph amesema kituo hicho kina faida huku wakimuomba Waziri Dkt. Dorothy kiboreshwe zaidi ili kutoa huduma kwa ufanisi na watoto wapate elimu bora zaidi.
“Rai na wito wangu tuwahimize wazazi kuleta watoto wengi zaidi, Waziri tunakuomba tusaidie mapungufu yaliyopo uliyoyaona hapa yarekebishwe, ulinzi upo vizuri mtoto akiwa huku shuleni mzazi unafanya kazi zako kwa urahisi na mama anapata muda wa kupumzika au kufanya kazi vizuri zaidi na mtoto anapata elimu,” alisema mkazi wa Gezaulole, Simon.
“Kituo kimewasaidia watoto wengi eneo hili walikuwa wanashinda kwenye vumbi na wazazi wao, mama anatoka na mtoto mdogo anaenda kufanya naye kazi kama ni biashara anazunguka naye juani, hiki kituo kimempunguzia adha ya lile vumbi hata kama amepata athari haitakua kubwa sana. Tunashkuru kwa kututengenezea kituo hiki. alisea mmoja wa mkazi wa eneo hilo Hadija Khamis
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa