Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo hii leo amepokea msaada wa vifaa tiba vilivyogharimu zaidi ya Shilingi Milioni Mia Nne kutoka kwa Shirika lisilo la Kiserikali la ESSO na kuzindua jengo la Huduma ya Uzazi na Mtoto lililogharimu kiasi cha Shilingi Milioni Mia Mbili Hamsini lililojengwa kwa ufadhili wa KOFIH (Korea Foundation for International Health)
Akizungumza na wananchi mara baada ya kupokea vifaa hivyo Waziri Dkt. Jafo amesema azma ya Serikalini ni kuhakikisha huduma na miundombinu ya Afya inaimarika na kutoa msukumo wa dhati katika kusogeza huduma bora kwa wananchi kwa kuimarisha mifumo ya utoaji huduma.
“Nawashukuru kwa dhati wadau hawa waliochangia huduma hizi za afya hapa Kisarawe, jengo hili limekamilika na limetumia fedha kiasi kidogo, hapa tunaona thamani halisi ya pesa iliyotumika, jingo ni zuri na limefungwa vifaa vya kisasa kabisa” Jafo alisisitiza.
Mwakilishi wa Shirika lisilo la Kiserikali la ESSO Bw. Raphael Gasper amesema kontena lenye urefu wa futi 20 limewasili kutoka Switzerland likiwa na vifaa tiba aina tofauti ikiwa ni pamoja na vitanda vya wagonjwa, mashine za kisasa kwa ajili ya matibabu ya moyo ambazo zinatarajiwa kunufaisha vituo vya afya 38 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe.
Nae Mwakilishi Mkazi wa KOFIH (Korea Foundation for International Health) Bw. Sung Ha amesema Taasisi yake itaendelea kusaidia uboreshaji wa vituo vya afya na huduma za Mama na Mtoto nchi ikiwa ni pamoja na kukarabati majengo ya kujifungulia, kununua magari ya dharula na kudhamini mafunzo mbalimbali kwa wataalamu wa Usingizi.
Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ina jumla ya vituo 42 vya kutolea huduma ya afya na takwimu zinaonyesha vifo vya akina mama vitokanavyo na matatizo ya uzazi vimeendelea kupungua kutoka vifo 15 mwaka 2017 hadi vifo 3 ilipofika Desemba 2021.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa