November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mvua zakwamisha ujenzi
wa barabara Ruvuma

Na Cresensia Kapinga,TimesMajira,Online Songea.

BAADHI ya wakandarasi mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kuwaongezea muda wa kufanya kazi za ujenzi wa barabara kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo kusababisha ujenzi kuwa mgumu.

Hayo wameyasema jana na baadhi wakandarasi wakati wakizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.

amesema kuwa mvua zimekuwa nyingi jambo ambalo limekuwa gumu katika ukamilishaji wa miradi.

Akizungumza kwa niaba ya wakandarasi wenzake Mkurugenzi wa Kampuni ya Jambera Campan Limited, Jems Mbeya amesema barabara nyingi za vijijini zimekuwa na mito mikubwa na madaraja hayawezi kuhimili kupita magari makubwa kwa ajili ya kupeleka malighafi za ujenzi ikiwemo makalavati.

Mhandisi Johnson Kweka akionesha moja ya calavat lililojengwa kwa ajili ya kutolea maji yasiendelee kuharibu barabara ya Kizuka, Mipeta, Muhukuru yenye urefu wa kilometa mita 30 Songea Vijijini.

“Mvua zimekuwa ni changamoto kubwa kwetu ambazo zinakwamisha kazi kwa kiasi kikubwa, tunashindwa kupeleka vifaa vya kujengea kama mchanga, kokoto na magari makubwa inakuwa ngumu kupita kwenye barabara hizo,” amesema Mkandarasi Jemes.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Wilaya ya Songea, mhandisi John Ambros alisema kwa sasa wanaendela na kuchonga barabara, kuweka makalavati pamoja na mifereji ili barabara za vijijini zisijifunge na kupitika kipindi chote cha mvua licha ya kuwa mvua ni kikwazo, lakini wanahakikisha hakuna barabara itakayojifunga

Amesema TARURA Songea kupitia Halmashauri ya Songea vijijini walipata pesa za mfuko wa jimbo kiasi cha sh. milioni 500 ambazo zinajenga barabara ya Kizuka, Mmipeta, Matama na Muhukuru barabarani yenye urefu wa kilomita 30, itakuwa na makalavati 20 yenye mita 7 pamoja na kilomita 10 za barabara zenye kiwango cha changalawe.

Ujenzi wa macalavat ukiendelea katika barabara ya Kizuka-Mipeta ambayo ni kubwa inayotegemewa na wakulima wa kata tatu kupeleka mazao yao sokoni.

Kwa upande wao wananchi wa vijiji vya Kizuka, Mipeta, Matama na Muhukuru wameiomba Serikali kuona umuhimu wa kuimarisha barabara za vijijini, kwani wanachi kwa sasa wanalima kwa wingi na ili waweze kupeleka mazao yao sokoni ni lazima barabara ziweze kupitika kipindi chote.