November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya huduma 10 za kibingwa zinatolewa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Zaidi ya Huduma za kibingwa 10 zinatolewa katika hospitali ya rufaa Mkoa wa Dodoma pamoja na Madaktari bingwa 29 na wahudumu wengine wa Afya wanaendelea kutoa huduma katika hospitali hiyo.

Hayo yamebainishwa leo na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Ernest Ibenzi wakati wa kipindi cha Mirindimo kinachorushwa na TBC Taifa.

“Katika hospitali hii tuna mabingwa kutoka katika vitengo mbalimbali wapo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na kuwafanya wanakuwa salama kiafya.” amesema Dkt. Ernest

Aidha, Dkt. Ibenzi ameishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayofanya haswa katika sekta ya Afya nchini na kuiangalia kwa karibu hospitali ya rufaa Mkoa wa Dodoma.

“Zamani tulikua tunawapeleka wagonjwa kupata huduma katika hospitali nyingine lakini kwa sasa huduma karibu zote na zile za kibingwa zinapatikana katika hospitali hii.”amesema Dkt. Ibenzi

Amesema kuimarishwa kwa huduma katika hospitali hiyo imeleta mafanikio na mabadiliko makubwa kwenye sekta ya afya nchini na hivyo wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani hupatiwa huduma hizo hapa Dodoma

Kwa upande wake Dkt. Samwel John ambaye ni mtaalamu wa Mifupa katika hospitali hiyo amesema wanapokea wagonjwa waliopata ajali, waliotibiwa na kupata Rufaa kutoka ndani ya Mkoa na mikoa jirani.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuboresha huduma pamoja na upatikanaji wa vifaa Tiba/Kinga kama vyuma na vifaa vya kutengenezea vifaa bandia.”amesema Dkt. John

Shuhuda ambaye alikua mgonjwa wa kuwekewa mguu bandia ndugu Augustino Makule amesema baada ya kufika katika hospitali hiyo hakua na fahamu lakini baada ya kupata fahamu ndani ya siku mbili akajikuta tayari ameshafanyiwa huduma nzuri na za haraka.

“Kuhusiana na Magonjwa ya Mifupa kiukweli hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma ipo vizuri maana baada ya kupata fahamu ikabidi niendelee na huduma kisha nikawekewa mguu bandia nashukuru naendelea vizuri.”amesema ndugu Makule

Miongoni mwa huduma zinazotolewa katika hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma ni pamoja na huduma za Tiba kifua kikuu, Huduma za chanjo, Masikio, pua na koo, huduma za macho, kinywa na Meno pamoja na huduma za Magonjwa ya wanawake na uzazi.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Ernest Ibenzi akielezea kifaa cha kuongeza hewa ya Oksjeni kwa mgonjwa kilichofungwa kwenye hospitali hiyo
Afisa mtekinolojia viungo tiba saidizi Bw. Festo Mgata akieleze namna ya vifaa hivyo vinavyotengenezwa hadi kufikia hatua ya kumuwekea mgonjwa katika hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma.
Wataalam wa Idara ya Mifupa wakielezea namna Ovena inavyofanya kazi ya kutengenezea viungo bandia