Na Joyce Kasiki, Dodoma
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amepiga marufuku vyuo na shule zenye wanafunzi wa kidato cha sita zitakazofunguliwa Juni 1, mwaka huu kutumia Corona kama kitega uchumi kwa kuanza kuagiza wanafunzi kwenda na vitu ambavyo havipo kwenye mwongozo wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee Watoto.
Pia imeonya wanafunzi kuanza kudaiwa ada wakati walikuwa wameishalipa ada kabla ya kufunga shule, kwa hiyo walikwenda nyumbani kwa sababu kulikuwa na changamoto ya ugonjwa.
Onyo hilo limetolewa leo na Prof. Ndalichako wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma. “Watu waache kutumia Corona kama kitega uchumi kwa kuanza kuagiza fedha za ziada. Fedha za kwa kazi gani? Wanafunzi walikuwa wameishalipa ada kabla ya kufunga shule , kwa hiyo walikwenda nyumbani kwa sababu kulikuwa na changamoto ya ugonjwa,” amesema.
Waziri Prof. Ndalichako amekemea vikali vyuo na shule hizo kuanza kuainisha vifaa mbalimbali vya wanafunzi kwenda navyo bila kuzingatia mwongozo uliotolewa na Wizara ya Afya.
Amesema sio kila chuo au shule kinatakiwa kuutoa mwongozo wake, ikiwemo kuwataka wanafunzi kwenda na spriti, tagawizi na vitu vingine, badala yake unaotakiwa kufuatwa ni mwongozo wa Wizira ya Afya.
Profesa Ndalichako ametaja mambo muhimu yaliyosisitizwa kwenye mwongozo huo wa Wizara ya Afya ni kuhakikisha kunakuwa na maeneo maalum ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni. Ametaja maeneo hayo kuwa ni mageiti, madarasa na kwenye mabweni.
“Katika mwongozo ambayo umesainiwa na Waziri wa Afya unasisitisa kunawa kwa maji tiririka na sabuni ndiyo iwe njia kuu na suala la vitakasa mikono liwe ni suala la hiari, lakini sio lazima, lakini kama vitakasa mikono vitakuwepo basi wazingatie vile vigezo ambavyo vimewekwa,” amesema Prof. Ndalichako.
Amesema Wizara ya Afya imekataza kupeleka spriti shule shuleni, kwanza inaweza kuwaka moto ikaunguza moto, lakini pia ni kilevi.
Pili amesema Wizara imesisitiza na kushauri wazazi kuwapatia watoto wao barakoa ambazo zimeshonwa kwa kitambaa ambazo mwanafunzi anaweza akafua akapiga pasi.
Amefafanua kwamba wanafunzi wanapoenda shuleni wazingatie umbali kati ya mtu na mtu, wajiepushe na misongamano iwe ni katika majadiliano, kwenye mabweni na wakati wa kula.
Amesema ni muhimu wakazingatia taratibu ambazo zinatolewa na Wizara ya Afya na watahakikisha taasisi zote zinaupata mwongozo huo.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja