November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ditopile: Rais Samia anazidi kuwafunga midomo waliombeza uendelezaji wa miradi Dodoma

Na Penina Malundo, Timesmajira, Online

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma,Mariam Ditopile amesema ndani ya muda mfupi madarakani wa Rais Samia Suluhu Hassan unazidi kuwaumbua wale waliombeza kuhusu uendelezaji wa miradi ya kimkakati Jiji la Dodoma iliyoasisiwa na Mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Mbunge Ditopile ameyasema hayo leo baada ya Hafla ya Rais Samia kuweka Jiwe la Msingi mradi wa Ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje katika mji wa Dodoma, ambapo barabara hiyo itatoka Ihumwa-Matumbulu-Nala-Veyula-Ihumwa yenye urefu wa Kilometa 112.3.

Mbunge Ditopile amesema Rais Samia anaonyesha kwa Vitendo na anayonia ya dhati ya kuendeleza miradi yote ya mtangulizi wake Hayati Dkt John Magufuli.” Nawasihi watanzania tupuuze maneno ya watu wachache wasioitakia mema Nchi yetu, Rais Samia atatekeleza miradi yote aliachiwa tena kwa kasi kubwa na ufanisi,”amesema Ditopile

Aidha amesema anampongeza Rais Samia kwa kuendelea kutimiza ahadi zake kwa vitendo za kuendeleza miradi yote ya kimkakati iliyoasisiwa na Hayati Dkt. Magufuli Jijini Dodoma, kwani miradi hiyo inaendelezwa kwa kasi kubwa.

“Yalikuwepo Maneno kwamba Hayati ameondoka na miradi itasimama au haitafanyika lakini sasa ni tofauti, miradi yote inaendelezwa…Mradi huu wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa Jiji la Dodoma ni mradi ulisubiriwa kwa Hamu na wana Dodoma utalibadilisha hili jiji letu”amesema na kuongeza

“Mradi mwingine unaendelezwa na Rais Samia Jijini Dodoma ni ujenzi wa Hospitali Mpya ya Jiji la Dodoma na tayari Rais Samia ametoa zaidi ya Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wake kuanza, sisi wana Dodoma tunamshukuru na kumpongeza Sana”amesisistiza Mbunge Ditopile

Ametolea mfano miradi inayotekelezwa ni pamoja na mradi wa Njia mchepuo Kusini Jiji la Arusha 42.4KM,Barabara ya Mbinga-Mbamba Bay 66KM,Barabara ya Singida-Babati-Minjingu 223.5KM,Barabara ya Arusha-Namanga 105KM,Iringa- Dodoma 260KM,Barabara ya Namtumbo-Tunduru 190KM.

Miradi mingine ni barabara ya Mayamaya-Bonga 188KM,Tunduru – Mangaka Mtambaswala 202.5KM yote inaendelea kutekelezwa na itakamilika kwa wakati katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia.