Na Penina Malundo, Timesmajira Online
KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Shaka Hamdu Shaka, amesema ndani ya miaka 45 tangu kuzaliwa kwa CCM, kimekuwa kinara kwa kuchochea mageuzi wa demokrasia Afrika kwa kuendelea kupiga vita siasa chafu zenye mlengo wa ubaguzi.
Amesisitiza CCM kitaendelea kuwa Chama sikivu, makini na kujali dhima ya majadiliano kwa njia za kiungwana kuliko kuandamwa na vitisho, kebehi, ubabe au kushuritishwa.
Akizungumza leo na waandishi wa habari wilayani Musoma, Mkoa wa Mara kuhusu mafanikio ya chama hicho kikongwe barani Afrika ndani ya miaka 45 tangu kilipozaliwa baada ya kuungana vyama vya TANU na Afro-Shiraz Party (ASP), mwaka 1977, amesema
CCM kipo tayari kupokea maoni, ushauri na maafikiano yanayoheshimu njia za kiungwana na kistaarabu kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Kazi kubwa ya utekelezaji wa sera kwa miaka yote ya utawala wa CCM madarakani ni kuhakikisha umoja wa kitaifa unadumu na kubaki, tukipinga siasa chafu za ukabila, rangi, dini au ukanda badala yake sera zake zimekuwa zikihimiza umoja na mshikamano hali ambayo imelifanya Taifa letu kuwa lenye utulivu, upendo na ushirikiano .
Akizungumzia mafanikio ambayo CCM inajivunia tangu kuzaliwa kwake, Shaka amesema katika kipindi hicho Chama kimeendelea kuwaongoza Watanzania katika kulinda uhuru wa nchi yao na harakati za kujiletea maendeleo yao.
Amesema mafanikio ya dhahiri yameonekana kupitia utekelezaji wa sera zake mbalimbali na kujijengea uhalali wa kuongoza nchi katika dunia ya sasa yenye mazingira yanayobadilika kila mara.
“Moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana ni kudumu na kuimarika kwa muungano wetu. Katika kipindi cha miaka 45 iliyopita muungano wetu umezidi kuimarika kutokana na juhudi za makusudi za chama chetu kuhakikisha muungano wetu unadumu milele,”amesema
Amesema wameweza kufanya mambo kadhaa mapya ambayo yamefanya mambo yaende vizuri zaidi. Kitendo cha kuungana kwa TANU na ASP ndiyo kilichozaa chombo kilichokuwa na nguvu na uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na changamoto za muungano wetu.
“Tutaendelea kuimarisha muungano wetu kwa faida ya nchi yetu na watu wetu. Tunafanya hivyo kwa kutambua faida kubwa na nyingi zinazotokana na muungano wetu ambazo kila mmoja wetu anazitambua,” amesema.
Shaka amesema kuwa mafanikio mengine ambayo chama kinajivunia kuimarisha umoja wa kitaifa kama ilivokuwa kwa vyama vya TANU na ASP ambapo sera za CCM zimeendelea kulenga katika kuwaunganisha Watanzania na kujenga taifa moja imara lenye watu wamoja.
Amesema licha ya tofauti za kisiasa, rangi, dini au kabila, kila mmoja anajivunia na kuona faraja kuwa Mtanzania na kuendelea kuimarisha amani, utulivu na mshikamano, mambo ambayo baadhi mataifa ya Afrika na hata duniani ni bidhaa adimu.
Amesema tumeweza kufanikiwa kubaki kuwa na taifa lenye umoja na utulivu, licha ya nchi yetu kupitia katika kipindi kigumu cha mageuzi ya kisiasa na kiuchumi na kuingia katika mfumo wa vyama vingi na uchumi wa soko huria.
“Watanzania ni watu wasioyumba wala kubabaishwa. Ni watu makini, wachambuzi na watambuzi mahiri. Haya ni mafanikio makubwa na ni jambo la kujivunia. Lakini pia ni sifa kubwa kwa chama chetu ambacho ndicho kiliongoza mageuzi hayo hapa nchini. CCM itaendelea kuimarisha dhamira yetu ya kudumisha na kuendeleza umoja, amani na utulivu wa taifa letu,” amefafanua
Kwa mujibu wa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Shaka amesema taifa limepiga hatua hatua na kupata mafanikio mbalimbali katika nyanja za kiuchumi na kijamii.
“Pamoja na kuwa bado nchi yetu ni maskini, lakini hali za watu wetu ni bora zaidi sasa kuliko ilivyokuwa mwaka 1977. Watu wengi wana kipato kikubwa, wanaishi katika nyumba bora zaidi, wanavaa vizuri na wanakula vizuri. Utoaji wa huduma za elimu, huduma za afya, maji, barabara, umeme zimeimarika kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Haya yote yanatokana na sera sahihi na mipango mizuri ya Chama cha Mapinduzi.
Akizungumzia CCM kuwa Mwalimu wa Demokrasia Shaka amesema Kuhusu demokrasia, alieleza kuwa CCM imekuwa mwalimu wa Demokrasia nchini, mataifa jirani na kimeweza kusimamia na kuongoza nchi kufanya uchaguzi, wananchi kutumia mamlaka na haki zao za kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka kwa amani na Utulivu.
Aidha, amesema CCM ndani ya miaka 45 imefanikiwa kusimamia muundo wa sera, mikakati na aina ya siasa inayohitajika katika nyakati za sasa jambo lililosaidia kulinda na kusimamia usalama wa taifa na watu wake ili kudumisha amani, umoja na kujivunia uhuru wake .
Amesema kazi kubwa ya utekelezaji wa sera kwa miaka yote ya utawala wa CCM madarakani ni kuhakikisha umoja wa kitaifa unadumu na kubaki, kupinga siasa chafu za ukabila, rangi, dini au ukanda badala yake sera zake zimekuwa zikihimiza umoja na mshikamano hali ambayo imelifanya taifa kuwa lenye utulivu, upendo na ushirikiano.
“Katika nyakati zote kila mwananchi amekuwa mlinzi wa Taifa lake, askari wa mstari wa mbele anayehakikisha hatokei adui akayejivisha koti la kuwa kibaraka au wakala, badala yake mapambano yameelekezwa dhidi ya maadui ujinga, umasikini na maradhi,” amesisitiza.
USHIRIKIANO KISIASA
Shaka amesema kwa miaka yote 45 CCM kimekuwa kuwa mstari wa mbele kuendeleza na kudumisha ujirani mwema ili kujenga haiba ya maendeleo ya kisiasa, kijamii, kiuchumi, kudumisha mahusiano mema, kuendeleza ushirikiano na vyama vingine rafiki na vya kidugu duniani ikiwemo kanda ya Afrika Mashariki.
Amesema kuwa CCM kimeendeleza mahusiano hayo ili kuhakikisha ujirani mwema unadumu, unaendelezwa kwa kuwaletea manufaa wananchi wa Tanzania na mataifa mengine.
Vilevile, amesema CCM katika kipindi cha miaka 45 kimekuwa chachu ya kuanzishwa kwa kamati ya nchi tano zilizo mstari wa mbele kusini mwa Afrika, kipindi ambacho mataifa kadhaa yalikuwa bado hayajapata uhuru.
Kwa kushirikiana na vyama vingine vya ukombozi, CCM kimekuwa na mchango kwa mataifa hayo kushamirisha juhudi za ukombozi hadi mataifa hayo yalipopata uhuru na kujitawala yenyewe.
Amesema dhana ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ni kutanuka kwa wigo wa demokrasia shirikishi, ushindani wa sera kwa sera, ujenzi wa hoja kwa nguvu ya hoja. Kwa kipindi chote cha miaka 45 CCM kimeendelea kuwa Chama sikivu na makini kwa nyakati zote.
“Kinapenda na kujali dhima ya majadiliano kwa njia za kiungwana kuliko kuandamwa na vitisho, kebehi, ubabe au kushuritishwa,”amesema
“CCM kipo tayari wakati wote kupokea maoni, ushauri na rai hatimaye kufikia kwa maafikiano yanayoheshimu njia za kiungwana na kistaarabu kwa maslahi mapana ya taifa letu,” amesema Shaka
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja