January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya CRDB imetoa zawadi kwa washindi wa promsheni yake ya TemboCardVisa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Benki ya CRDB imetoa zawadi kwa washindi wa promsheni yake ya TemboCardVisa ijulikanayo kama “Tisha na TemboCardVisa” katika hafla fupi iliyofanyika katika makao makuu ya Benki hiyo yaliyopo barabara ya Ali Hassan Mwinyi Jijini Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo jumla ya washindi 7 wamekabidhiwa zawadi zao ikiwamo zawadi za tiketi za kwenda Cameroon kushuhudia michuano ya AFCON kwa washindi wanne. Wakati washindi wengine 3 walikabidhiwa zawadi mbalimbali ikiwamo safari ya utalii Zanzibar, ‘home-theater’, televisheni, pamoja na simu ya mkononi ya iphone 13 pro max.

Akizungumza katika hafla hiyo ya utoaji zawadi Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa aliwapongeza washindi wa kampeni hiyo huku akiwahamasisha wateja wengine kushiriki kwani kampeni hiyo bado inaendelea mpaka mwezi April. “Niwapongeze sana washindi wetu, na niwaombe muendelee kutumia kadi zenu za TemboCardVisa na mkawe mabalozi pia kwa ndugu jamaa na marafiki zenu ili siku nyingine nao tuwaone wakishinda,” alisema Raballa.

Raballa alisema promosheni hiyo ina lengo la kuwahamasisha wateja wa Benki ya CRDB na Watanzania kufanya malipo na manunuzi kwa kutumia kadi zao za TemboCardVisa. “Lengo letu ni kuwajengea wateja wetu utamaduni wa kutumia kadi zao kufanya malipo na manunuzi mitandaoni ‘online shopping’ na kupitia vifaa vya manunuzi vilivyopo sehemu mbalimbali kama supermarkets, maduka ya rejareja, mahotelini, mahospitalini, migahawa na taasisi nyingine mbalimbali binafsi na za serikali,” alisema Boma.

Promosheni ya “Tisha na TemboCardVisa” ilizinduliwa rasmi mapema mwezi wa kumi na mbili (12) kwa Benki ya CRDB kushirikiana na Visa International ambao pia ni moja ya wadhamini wa michuano ya AFCON yanayoendelea nchini Cameroon. Kupitia promosheni hiyo ya “Tisha na TembocardVisa,” Benki ya CRDB imekuwa ikitoa zawadi kwa wateja ambao wamekuwa wakifanya miamala mingi zaidi ya malipo kupitia kadi zao.

Mpaka sasa Benki ya CRDB imeshatoa zawadi kwa wateja 127, ikiwamo wanafunzi 15 ambao wameshinda simu za mkononi aina ya Samsung, wateja 100 ambao walirudishiwa shilingi 100,000 kila mmoja katika manunuzi ya tiketi za ndege waliyoyafanya, pamoja na wateja 5 ambao walilipiwa bili ya malipo ya manunuzi yao yaliyofuata (next bill) ya shilingi 500,000 kila mmoja.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Kadi Benki ya CRDB, Farid Seif, alisema imekuwa ni fahari kuona jamii imekua na mwitikio mzuri na kusema kuwa mwitiko huo unadhihirisha namna jamii inavyoelimika juu ya kupunguza matumizi ya fedha taslimu na kutumia mifumo ya kidigitali kufanya malipo na manunuzi katika kukidhi mahitaji yao mbalimbali.

“Mwitikio huu unaongeza chachu kubwa katika kuleta mapinduzi katika sekta ya fedha pamoja na kuiweka nchi yetu kwenye ramani ya dunia ya nchi zinazotumia teknolojia za kisasa kujenga utamaduni wa “cashless economy” jambo ambalo linatufanya tuendelee kuboresha huduma zetu tunazozitoa,” alisema Seif huku akibainisha kuwa Benki hiyo imefanya mabresho ya TemboCard ambapo sasa hivi zina muonekano wa kisasa na zinampa mteja urahisi wa kutumia.

Akizungumza kwa niaba ya wateja walioshinda safari ya AFCON, Njama Matumbo aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuendesha promosheni hio ya “Tisha na TemboCardVisa” ambayo si tu inalenga katika kuwazawadia washindi wanaopatikana lakini pia kuelimisha jamii kuendana na dunia tuliyopo ya kutumia mifumo ya kisasa ya kidigitali kufanya malipo na manunuzi, na kuondokana na zana ya kutembea na fedha taslimu.

Kwa mara ya kwanza Benki ya CRDB ilizindua huduma ya TemboCard mwaka 2002, ikilenga kuwapa wateja wake urahisi na unafuu wa upatikanaji wa huduma popote walipo kupitia kadi hizo za TemboCard. Mpaka sasa Benki ya CRDB imefanikiwa kuingiza katika soko zaidi ya TemboCard milioni 4. Urahisi, usalama na unafuu wa huduma ya TemboCard unawawezesha wateja wengi wa Benki ya CRDB kufanya malipo ya bidhaa na huduma mbalimbali bila kuhitaji fedha taslimu.