January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashabiki sita wa Simba wapata ajali Kahama

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MASHABIKI sita timu ya Simba wamejeruhi baada ya gari aina ya Coaster waliyokuwa wakisafiria kwenye Bukoba kushudia mpambano wa timu yao dhidi ya Kagera Sugar kupata ajali.

Habari zilizopatikana leo zilieleza kwamba ajali hiyo ilitokea kwenye Kijiji Mwendakulima kilichopo kwenye Hifadhi ya Msitu wa Serikali wa Mkweni, wilayani Kahama.

Miongoni mwa waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni wanaume wanne na wanawake wawili na wote wamelazwa Hospitali ya Kahama wakipatiwa matibabu.

Simba inatarajia kucheza mchezo wake wa kiporo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Kagera kesho. Mchezo huo unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba. Mchezo huo unatarajia kuwa wa kufa na kupona kwa timu zote mbili, hasa baada ya Simba kutokuwa na matokeo mazuri.

Simba itakuwa na kibarua kigumu cha kuanza kupunguza pointi 10 ambazo inazidiwa na watani wake wa jadi Yanga ambao ndio vinara wa Ligi hiyo kwa pointi 35 dhidi ya 25 za Simba.

Simba itajitupa kwenye Uwanja wa Kaitaba huku ikiwa na redi ya kutofanywa vizuri kwenye michezo yake miwili iliyopita, ambapo katika mchezo wa dhidi ya Mbeya City ilipata kipigo cha bao 1-0 kabla ya kutoshana nguvu na Mtigwa Sugar kwa sara ya 0-0.

Kutokana na matokeo hayo yasiyofurahisha, Simba itajitupa uwanjani ikiwa na kibarua cha kuwapa raha wapenzi wake ambao kwa takribani wiki mbili sasa wamekuwa wakikosa raha kwa timu yao kufanya vibaya.

Gari iliyokuwa imebeba mashabiki wa Simba kutoka Kahama kwenda mkoani Kagera iliyopinduka katika kijiji cha mwendakulima kwenye hifadhi ya serikali ya msitu wa mkweni.