Na Ansel Missango
ASILIMIA kubwa ya Watanzania hivi sasa wanaenda na wakati katika matumizi ya kidigitali.
Kuna mifano mingi kama vile matumizi ya simu za mikononi,kompyuta, pamoja na vitu vya nyumbani kama vile televisheni janja, michezo ya kompyuta nakadhalika.
Mjadala mkubwa umeibuka pamoja na maswali mengi kuhusiana na kiasi gani au kwa namna gani mamlaka husika zitakavyoweza kuongeza mapato kwa kupata kodi ya VAT katika huduma za kidigitali.
Nchi za wenzetu,kodi katika huduma za kimtandao hujulikana kama ‘Google Tax’.Katika utandawazi, idadi kubwa ya miamala kutoka maeneo mbalimbali ulimwenguni ni jambo la kawaida kukatwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Msingi huo ndio umeandaliwa ili kuhakikisha kuna usawa wa kibiashara duniani kwa kuhakikisha bidhaa zinapovuka mipaka zinakatwa kodi kutokana na makubaliano yaliyopo.
Utekelezaji wa jambo hili unafikiwa kwa kukata kodi bidhaa zinazoingia nchini pamoja na zile zinazosambazwa ndani ya nchi.
Lengo hilo husaidia bidhaa zinazokwenda nje ya nchi kutokuwa na VAT ili kutoa nafasi kwa nchi zinazopokea bidhaa hizo zipate fursa ya Ongezeko la Thamani(VAT).
Kimsingi kuna makubaliano duniani kuwa nchi ya mwisho kupokea bidhaa na huduma,ndio yenye fursa ya kukata kodi katika miamala ya kimataifa, changamoto kubwa ya utekelezaji, inaweza kuwa ni huduma yenyewe ikishavuka mipaka, kwani inaweza kuwa imeshakufa(expire) hivyo kukwamisha udhibiti na kupatiana kwa kodi kupitia mamlaka za kikodi mipakani.
Pia watoa huduma ambao si wakazi wa nchi husika, mara nyingi hawana anwani zinazotambulika. Hata mhusika kujikadiria kiwango cha kodi, ili kulipa kodi kutokana na huduma anayolipia, imeshindwa kutokana na kutofahamika uhalisia na chanzo cha huduma husika.
Kwa miaka mingi sasa, changamoto hizi hazikuwahi kuwa tatizo kwa sababu ya uchache wa huduma zilizokuwa zikuvuka mipaka na kuingia nchini.
Pamoja na kiwango kidogo cha mapato,nchi nyingi aidha hazikuingiza kutoza kodi huduma hizo au kutoona umuhimu wa kukusanya kodi katika miamala hiyo.
Kutokana na idadi kubwa ya bidhaa za kidigitali, miaka ya nyuma nchi nyingi duniani kupitia mawakala wa kodi ziliona umuhimu wa kutoza kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika bidhaa na huduma za kidigitali.
Matokeo yake, wasiwasi umezidi kuongezeka kutokana na kiwango kidogo au kutokuwa na mapato kabisa yanayokusanywa kupitia kodi katika bidhaa na huduma za kidigitali.Wakati huo kuna biashara ndogo ndogo ambazo zilitakiwa kulipa kodi na huingizwa sokoni na kushindana huku zikiwa na unafuu mkubwa zikifananishwa na zile ambazo zinalipa kodi.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2019 za Shirika la Umoja wa Mataifa Maendeleo na Biashara (UNCTAD), Tanzania inaingiza huduma za kidigitali zenye thamani ya dola za Marekani milioni 317 kwa mwaka.
Kwa kiwango hicho cha mapato, kuna asilimia 18(VAT) sawa na dola za Marekani milioni 57 zinapotea kila mwaka. Kwa sasa hakuna namna ya kudhibiti makusanyo ya huduma zinazoingia nchini hivyo kupotea kwa kiwango kikubwa cha mapato nchini.
Kwa kuwa nchi nyingi duniani tayari zina mifumo inayofanyakazi katika kukusanya kodi ya VAT, bila shaka ni wakati sahihi kwa Tanzania sasa kupiga hatua nyingine kama taifa kwa kuiga mifano nchi nyingine duniani.
Mwandishi wa Makala hii ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Great Mobile Tech Solutions, iliyopo Masaki, jijini Dar es Salaam. Missango ana uzoefu mkubwa katika masuala ya teknolojia, benki pamoja na teknolojia ya fedha(Fintech).
Kabla ya kuanzisha kampuni yake inayohusika na masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano, Missango amewahi kufanya kazi katika moja ya makampuni makubwa duniani kama Mtendaji Mkuu ambapo alipata uzoefu wa kutosha katika sekta ya digitali pamoja na mambo mengine.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani